UMOJA wa Mataifa nchini Tanzania unaendelea na uelimishaji wa wananchi kuhusu malengo ya Dunia yaliyoelezwa katika Maendeleo Endelevu (SDGs), malengo ambayo sasa yana takribani mwaka mmoja.

Ili kuweza kufikisha malengo hayo kila mahali , Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na serikali utatumia wiki ya vijana kufundisha wanafunzi 400 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Simiyu ili wawe wakufunzi kwa wenzao.

Mafunzo hayo yamelenga kuwafanya vijana kuelewa na kuongeza ufahamu kuhusiana na malengo hayo ya dunia, hivyo kuwasaidia wenzao na wananchi wengine kutambua wajibu wao katika utekelezaji wake.

Mafunzo hayo mkoani Simiyu ni mwendelezo wa mafunzo yaliyozinduliwa mkoani Arusha na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez.

Hadi sasa Umoja wa Mataifa umewezesha vijana 70 kutambua malengo hayo na kutumika kufunza wengine. Aidha wabunge zaidi ya 180 walipewa mafunzo hayo huku wahadhiri na wanafunzi 1,000 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakiwa nao wamenolewa kuhusiana na malengo hayo ya maendeleo endelevu.
Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Stella Vuzo akielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mashirika ya Umoja huo hapa nchini kwenye mafunzo ya siku moja ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa vijana wa mkoa wa Simiyu, yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Alliance mjini Bariadi mkoani Simiyu.

Mkurugenzi Msaidizi, Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia umaskini, sera na uchambuzi, Bw. Mudith Cheyo alichangia katika mafunzo hayo kwa kueleza ni kwa namna gani serikali inatekeleza malengo hayo ya dunia. Bw. Cheyo amesema “Asilimia kubwa ya nguvukazi ya taifa letu ni vijana hivyo basi ni muhimu sana kuwashirikisha katika utekelezaji wa Malengo Ya Dunia katika ngazi ya taifa. Asilimia 34 ya nguvu kazi ni vijana, serikali imepanga mikakati kuhakikisha vijana wanapewa uwezo wa kuwawezesha kuzitumia fursa zilizopo kuleta maendeleo.”

Alisema kwamba kuwafunza vijana kuhusu malengo hayo ya maendeleo endelevu ni sehemu ya utendaji wa serikali katika utekelezaji wa malengo.

Akizungumza katika semina ya malengo endelevu, Bw.Amon Manyama, Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja huo(UNDP), alisema ajenda ya maendeleo kuelekea mwaka 2030 inahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu hasa vijana.
Ofisa wa Mawasiliano na Ushirikiano NUNV kutoka Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Didi Nafisa akitoa utangulizi wa Malengo ya Dunia (Global Goals) kwa kundi la vijana wa Simiyu (hawapo pichani) katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika kwenye ukumbi wa shule ya Alliance mjini Bariadi mkoani Simiyu.

“Ni muhimu sana kwa vijana kuelewa Malengo ya Dunia. Huu ni wakati wao. Kwa kuyaelewa malengo haya inrahisisha utekelezaji wake. Nimefurahi kuona muamko wa vijana waliojitekeza hapa leo na natumaini watawafikishia wengine ujumbe huu.” alisema na kuwapongeza vijana hao 400 kwa ushiriki wao katika kujifunza na kuelewa malengo hayo ya dunia na wajibu wa kila mmoja wetu.

Septemba 2015, viongozi 193 kutoka nchi mbalimbali duniani walikubaliana kuhusu malengo endelevu 17 kuelekea mwaka 2030.
Mkuu wa Programu, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Amon Manyama akiwapiga msasa wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) vijana wa mkoa wa Simiyu wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyofanyika kwenye ukumbi wa shule ya Alliance mjini Bariadi mkoani Simiyu.

HABARI ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...