Afisa Mkuu Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Frank Kanyusi akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Alionya wafanyabiashara ambao hawajasajili majina ya biashara kufanya hivyo katika kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa au kuchukuliwa hatua za kisheria.


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa muda wa miezi miwili kwa wafanyabiashara wanaotumia majina ya biashara pasipo kusajiliwa wafanye hivyo haraka.

Akizungumza na waandishi wa waandishi wa jijini Dar es salaam  jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Frank Kanyusi alisema katika zoezi la kutoa elimu na kurasimisha majina ya biashara na kampuni linaloendelea katika mikoa mbalimbali imebainika kuwa wafanyabiashara wengi wanatumia majina ya biashara pasipo kuyasajili.

“Sheria ya majina ya biashara inamtaka mfanyabiashara kusajili jina la biashara yake ndani ya siku 28 toka aanze kulitumia,” alisema Bw.Kanyusi na kuongezea kuwa kinyume na hapo atakuwa amevunja sheria ya majina ya biashara.

Alisema baada ya muda huo kupita, patakuwa na msako nchi nzima ili kuwabaini wale wote wanaotumia majina ya biashara pasipo kusajili na kuwafikisha katika vyombo vya sheria au kuwatoza faini.

Alisema kuwa sasa usajili wa majina ya biashara umerahisishwa kwani unafanywa kwa njia ya mtandao kwa kutembelea tovuti ya wakala huo ambayo ni www.brela.go.tz ili kupata maelezo yote ya namna ya kusajili jina la biashara.

Aliwataka wafanyabiashara wasiishie kusajili tu jina la biashara bali pia waende katika Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa ajili ya kupata namba ya Mlipa Kodi (TIN) pia waendele katika halmashauri zao kupata leseni ya biashara.

“Kwa kurasimisha biashara serikali itapata mapato kwani wigo wa walipa kodi utaongezeka na pia itakuwa faida kwa wafanyabiashara katika kujengewa mazingira bora ya kufanya biashara,” alisisitiza Bw.Kanyusi.

Alisema BRELA imejipanga kuzunguka mikoa yote nchini ili kutoa elimu juu ya urasimishaji wa majina ya biashara na makampuni kwani imeonekana wananchi hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa urasimishaji.

Hadi sasa BRELA imefanya ziara katika mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Simiyu na wiki hii watakuwa mkoani Shinyanga kwa muda wiki moja katika kuhamasisha wafanyabiashara kurasimisha biashara zao.

Alisisitiza kuwa ni lazima kuhakikisha kuwa biashara zinarasimishwa ili serikali iweze kuwatambua walipa kodi wake ambao watachangia pato la taifa na kuiwezesha Tanzania kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. sasa mnasema tujisajili online, na mimi nimejaribu kujisajili inakataa kabisaa na hapo pembeni nimeangalia wameweka namba ambazo unaweza kupiga ukapata msaada, nimezipiga hazipokelewi! swali langu au ushauri unapokuwa umeweka tangazo jiandae kabla naona hawakujiandaa kwenye hili hawa brela

    ReplyDelete
  2. Brela huo usajili wa online bado link haifunguki kila ukigusa inakataa hivyo naomba mlifanyie kazi hili wengi WETU tunatimia sim za smart phone sio computer okoeni jahazi kwa kuturahisishia kuifungua hiyo link pia wekeni lugha ya kiswahili kwa watanzania wengi hawajui au kukielewa kingereza lugha ni muhumu kubadilishwa. Natanguliza shukrani

    ReplyDelete
  3. usajili wa online ni shida jamani,nisaidieni .Namba za msaada hazipokelewi

    ReplyDelete
  4. Namba za msaada mara nyingi hazipokelewi na zikipokelewa hawafanyii kazi maoni ya walalamikaji.
    Nimewahi mara kadhaa kulalamika kuhusu kibox cha "SUPPORT" kilichopo chini kabisa upande wa kulia wa dialogue box ya kusajili jina online. Unapofika mwisho na unataka kusubmit application kile kibox kinaziba execution instructions. Nilishawaeleza wahusika ambao namba zao zimewekwa lakini sijui hata kama huwa wanasikiliza seriously.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...