Timu ya soka ya Watumishi FC wilayani Kishapu Mkoa wa
Shinyanga imenyakua ubingwa wa michuano ya Mwenge wa Uhuru kuwania Kombe la
Ng’ombe.
Katika michuano hiyo iliyotimua vumbi jana jioni, timu
hiyo inayoundwa na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu iliibamiza kwa
mikwaju ya penati Igaga FC mabao 4-2.
Mchezo huo uliochagizwa na hamasa kutoka kwa mashabiki
ukichezwa uwanja wa shule ya msingi Mhunze, ulimalizika kwa dakika 90 huku ubao
wa matokeo ukisomeka 1-1 yaliyofanya mikwaju ya penati zipigwe.
Katika matokeo ya mikwaju ya penati timu hiyo ya
watumishi iliibuka kidedea na inatarajiwa kukabidhiwa zawadi yao ya ng’ombe
Ijumaa katika kilele cha Mwenge wa Uhuru wilayani humo.
Awali kabla ya mchezo wa fainali kulikuwa na mechi kati
ya Talents FC na Bodaboda zote za mjini Mhunze wilayani humo kutafuta mshindi
wa tatu.
Hadi refa anapuliza kipyenga cha mwisho Talents
walikuwa wameondoka na ushindi wa bao 1-0 na kuibuka washindi wa tatu.
Michuano ya kuwania kombe la ng’ombe ilianza wiki mbili
zilizopita wilayani humo ikiwa na lengo la kuwajengea vijana ari ya kujituma na
kujiletea maendeleo.
Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba alishuhudia mtanange huo akiwa
ameambatana na viongozi wengine akiwemo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri
hiyo, Stephen Magoiga Katibu Tawala Wilaya, Shadrack Kengese , Mkuu wa Polisi
wilaya, SP.E.Ulomi na Mshauri wa Mgambo Wilaya, SSgt.Charles Lyashimba.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga (kushoto) akibadilisha
mawazo na mwenyekiti wa Bodaboda wilayani humo, Daniel Eva.
Kocha
wa Watumishi FC, Japhet Makelele akitoa mawaidha kwa wachezaji wake wakati wa
kipindi cha mapumziko kwenye mchezo kati ya timu hiyo na Igaga FC.
Mchezaji
wa Watumishi FC mwenye namba 4 mgongoni akijaribu kuwatoka wachezaji wa Igaga
FC huku wachezaji wenzake wakijiandaa kutoa msaada.
Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo
waliojitokeza katika uwanja wa shule ya msingi Mhunze kushuhudia fainali za kuwania
kombe la ng’ombe kama shamrashamra za mbio za Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa
kuwasili wilayani humo Ijumaa ya Oktoba 7, 2016.
Wananchi
wa wilaya ya Kishapu wakishuhudia mtanange wa fainali hizo.
Mashabiki
wa Watumishi FC wakishangilia ushindi wa timu yao mara baada ya kupigwa kwa
mikwaju ya penati.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...