WAZIRI MKUU  Mhe. Kassim Majaliwa amepokea michango yenye thamani ya sh. milioni 660.25 zikiwa ni fedha taslimu, hundi na vifaa mbalimbali kwa ajili ya wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, mwezi uliopita. 
Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika leo mchana (Jumanne, Oktoba 11, 2016) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi hundi ya mfano kwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais wa kampuni ya ACACIA, Bw. Deodatus Mwanyika amesema wao wametoa sh. milioni 325 ambazo tayari wameshaziingiza kwenye akaunti ya maafa.
Amewaomba wadau wengine na taasisi nyingine hapa nchini wajitokeze kuisaidia Serikali kukabiliana na janga hili kwani mahitaji halisi ni makubwa kuliko kiasi ambacho kimekusanywa hadi sasa.
Wadau wengine waliochangia ni Balozi wa Japan nchini, Bw. Masaharu Yoshinda pamoja na Shirika la Misaada la Maendeleo la Japan (JICA) ambao wametoa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 220. Vifaa hivyo ni mahema 220, mablanketi 1,100; vigodoro vyepesi (sleeping pads) 1,110; madumu ya maji 250 na plastic sheets 22.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBC1, Dk. Ayoub Rioba ambaye alikabidhi hundi za sh. milioni 41.55, amesema kama taasisi waliguswa na tatizo la maafa ya Kagera kwa hiyo wakatafuta njia ya kuchangisha ili wapate fedha za kuisaidia Serikali kukabiliana na tatizo hilo.
“Tuliamua kufanya harambee na kuwahamasisha wananchi wachangie ambapo wengine walileta kwetu na wengine wakapeleka moja kwa moja Kagera. Na leo tunakabidhi kiasi ambacho tulikikusanya kupitia harambee hiyo,” amesema.
Wengine waliokabidhi michango yao, ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wenye Magereji Tegeta, Bw. Leonard Mwanjela ambaye ametoa fedha taslimu sh. milioni mbili kwa niaba ya mafundi gereji wilaya ya Kinondoni. Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Bw. Abdalla Mwinyi amesema walifanya harambee na kupata sh. milioni 60.8 ambazo wameamua kununua nguo na magodoro, unga wa mahindi tani 10.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa akipokea msaada wa mablanketi kutoka kwa Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida ukiwa ni msaada kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.Kulia ni Mwakilishi Mkuu wa Shirika la JICA nchini Toshio Nagase.
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 41.5 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC)  Dkt. Ayoub Ryoba ikiwa ni kutokana na harambee iliyofanywa na Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. 
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa akipokea moja ya misaada kutoka kwa Katibu wa Jumuiya ya wafanyabiashara wa kariakoo Bw.Abdallah Mwinyi ambao wametoa vifaa vyenye thamani ya milioni 60 ikiwa ni kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.
Picha na Daudi Manongi, MAELEZO. 

HABARI ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...