*Aagiza Baraza la Madiwani lipitie upya na kumpa majibu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma lifanye marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo ambayo imepandishwa kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
 Amesema anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

Amesema soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali nzuri na Manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza wafanyabiashara.

“Kwa kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na baraza la Madiwani, sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena katika baraza na muangalie namna ya kupunguza gharama hizo,” amesema.

“Hali hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi. Mkurugenzi wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini” amesisitiza.

Pia ameitaka Manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko hilo yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija na kuwataka Mkuu wa mkoa na wilaya kuwachukulia hatua wotewatakaobainika kuiba fedha hizo.

Amesema Manispaa hiyo inatakiwa kupanua masoko kwa kujenga masoko mapya makubwa katika maeneo ya Nkuhungu, Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili huduma hizo zisambazwe.

Mapema akisoma risala yake, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Godson Rugazama alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko hilo kuwa ni pamoja na ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na shughuli za wajasiriamali sokoni hapo. “Kodi imeongezeka kutoka sh. 20,000 hadi 150,000 kwa mwezi,” alisema.

Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa mifereji ya maji machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa katika maeneo yasiyokuwa rasmi na kusababisha wateja kutoingia sokoni.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali zikiwemo wodi za wagonjwa, jengo la wazazi na jengo jipya la wagonjwa wa Bima ya Afya (NHIF).

Akiwa hospitalini hapo, pia alizungumza na watumishi wa sekta ya afya na kuwataka wawahimize wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unawawezesha mtu kulipia bima ya matibabu kwa ajili ya mhusika, mwenza wake na watoto/watemezi wanne na serikali inajazia kiasi kile kile alichochangia.

Akizungumzia miundombinu ya afya mkoani humo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Dodoma hauna shida ya matibabu au utoaji wa huduma ya afya kutokana na miundombinu iliyopo hivi sasa.

Aliwataka wafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu na kuongeza tija katika utendaji kazi wao huku wakitanguliza utunzaji wa mali ya umma.

“Ninawasihi mjenge tabia ya huruma kwa wagonjwa huku mkitambua unyeti wa kazi mliyonayo. Ninaamini mtatunza vifaa mlivyonavyo na siyo kuvichukua na kuvipeleka kwenye zahanati zenu au maduka yenu binafsi ya dawa,” alionya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, OKTOBA MOSI, 2016
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wafanyabiashara wa soko Kuu la manispaa ya Dodoma la Majengo wakati alipolitembela Oktoba 1, 2016.
 Kama kawaida ya watanzania wengi siku hizi suala la matumizi ya mbango kama njia ya kuwasilisha ujumbe wao kwa viongozi  wafanyabiashara  hawakuzubaa  wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea soko kuu la manispaa ya Dodoma la majengo Oktoba 1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)  
 Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa   akitembelea soko kuu la Manispaa ya Dodoma la Majengo 
 Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa   akitembelea soko kuu la Manispaa ya Dodoma la Majengo 
 Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa   akitembelea soko kuu la Manispaa ya Dodoma la Majengo 
 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma  Jordan Rugimbana akimkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzungumza na wafanyabiashara wa soko kuu la Manispaa ya Dodoma la Majengo baada ya kulitembelea Oktoba 1, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wafanyabiashara wa Soko kuu la Dodoma la Majengo  wakati alipotembelea soko hilo Oktoba 1, 2016. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...