DHIBITINI BIASHARA ZA MAGENDO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi kuhakikisha anadhibiti wafanyabiashara wanaonunua korosho kwa njia ya magendo na atakayekamatwa achukuliwe hatua.

Pia amewataka wananchi wa mkoa huo kutouza korosho zao kwa walanguzi maarufu kangomba na badala yake wazipeleke kwenye masoko rasmi ili waweze kupata tija. “biashara ya kangomba ni mwiko atakayekamatwa amebeba korosho za kangomba atachukuliwa hatua za kisheria na chombo chake cha usafiri kitataifishwa” amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Oktoba 17, 2016) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa katika mikutano iliyofanyika kwenye vijiji vya Mibure, Namakuku, Ng’imbwa, Chienjele, Mkata, Mitope na Kitandi

“Marufuku kuuza korosho kwa kangomba kwani mnapata hasara kipimo kinachotumika si rasmi. Mkoa kamateni na taifisheni korosho na chombo cha usafiri kitakachotumika kubeba korosho za magendo,” amesema.Amesema ni vema wakulima wakaachana na biashara ya kangomba kwa sababu haina tija na badala yake wasubiri na kwenda kuuza korosho zao katika minada kwa bei nzuri.

“Mwaka huu korosho itauzika kwa bei ya juu zaidi isiyopungua sh.3500, msikubali kuuza korosho mlizizitolea jasho kwa walanguzi wanaotumia kangomba kwa sh. 1000 huu ni wizi, kwani kile kipimo cha wanachotumia ni sawa na kilo mbili, hivyo unapoteza zaidi ya sh. 6000”. amesema

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwasisitiza wananchi hao kuongeza idadi ya mazao ya biashara na kuanza kulima alizeti ambapo wataweza kupata faida ya zaidi ya sh. milioni moja kwenye shamba la ukubwa wa ekari moja. Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi ametoa miezi miwili kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue kuhakikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mibure unakamilika. “Ndani ya miezi miwili Zahanati iwe imekamilika, tuache kuzungumza sasa ni vitendo tu”amesema.

Awali Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kukamua mafuta ya ufuta na karanga cha Ilulu kilichoko wilayani Nachingwea na kukuta kimetelekezwa. Ameagiza uongozi wa kiwanda kumpelekea nyaraka zote za umiliki. Kiwanda hicho kilibinafsishwa kwa marehemu Abbas Gulamali na sasa kinasimamiwa na familia yake. “Nawahitaji Dodoma Oktoba 22 waje na nyaraka zao ili nijue walipokabidhiwa kiwanda hiki walitaka kufanya nini,” alimuagiza Msimamizi wa Kiwanda hicho Dinna Mavumbi kuwajulisha wahusika.

Waziri Mkuu alisema haiwezekani kiwanda hicho kilichojengwa kwa fedha za umma kikatelekezwa bila ya kuendelezwa. Alisema baada ya kupitia nyaraka zao ataangalia namna ya kurudisha majengo hayo ya kiwanda kwa Serikali. “Hatuwezi kuacha raslimali hii ikiwa imetelekezwa msituni inaharibika.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 17, 2016
koro1
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mkewe Mary Majaliwa wakiangalia kiwanda  cha ILULU kilichokuwa kinatengeneza mafuta ambacho muekezaji amekifanya kuwa Ghala nakukitelekeza na watu kuiba vifaa na kufanya uharibifu mkubwa Kiwanda hicho kipo wilaya ya Rungwe Mkoani Lindi Waziri Mkuu yupo katika ziara ya kikazi katika wilaya ya Nachingwea na Rungwe Mkoani Lindi(Picha na Chris Mfinanga)
koro2
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia baadhi ya magari yalivyo haribika ambayo yalikuwa yanamilikiwa nakiwanda cha kukamua ufuta  ILULU kiwanda hicho kipo wilani Nachingwea Mkoani lindi ambapo mwekezaji aliye kichukua amebadili matumizi na kukifanya Ghala lakuhifadhia bidhaa kushoto kwa waziri mkuu ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi    picha na Chris Mfinanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...