Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa mkurugenzi wa kiwanda cha Magodoro Dodoma, Haidary Gulamali, magodoro 200 yenye thamani ya shilingi milioni 10 ukiwa ni msaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Makabidhiano hayo yalifanyika baada ya Waziri Mkuu kutembelea kiwanda hicho Oktoba 2, 2016. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama Spring zinazotumika kutengeneza magodoro wakati alipotembelea kiwanda cha Magodoro Dodoma Oktoba 2, 2016. Kushoto ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Haidary Gulamali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kiwanda cha Magodoro Dodoma baada ya kutembelea kiwanda hicho Oktoba 2, 2016. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Haidary Gulamali na kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na wapili kulia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

MKURUGENZI wa kiwanda cha magodoro cha Dodoma Asili Bw. Haidary Gulamali amesema atawaleta madaktari bingwa 14 kuja kufanya upasuaji wa moyo bure kwa watoto watakaobainika kuwa na matatizo hayo.

Amesema madaktari hao ambao wanatarajia kuingia nchini hivi karibuni ataanzia kutoa huduma hiyo katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza na kisha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Bw. Gulamali ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kiwanda hicho akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

“Mtoto wangu amefanyiwa upasuaji wa moyo mara sita na Desemba atafanyiwa upasuaji mwingine nchini India. Nikiwa nchini India nimefahamiana na kujenga urafiki na madaktari wengi wa moyo kati yao 14 watakuja nchini na kutoa huduma ya matibabu hayo bure,” amesema.

Mbali na kupeleka madaktari hao katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, pia Bw. Gulamali ameahidi kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana magodoro mapya kwenye hospitali hiyo.

Wakati huo huo Bw. Gulamali amemkabidhi Waziri Mkuu magodoro 200 yenye thamani ya sh. milioni 10 kusaidia wananchi waliathirika na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 wengine 440 walijeruhiwa. Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

Waziri Mkuu alishukuru Bw. Gulamali kwa msaada huo na kuahidi kuwa  Serikali itahakikisha magodoro hayo inayafikisha Kagera kwa walengwa kama ilivyokusudiwa. Pia Waziri Mkuu alimpongeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho kwa uamuzi wake wa kuleta madaktari bingwa wa moyo kutoka India watakaotoa  huduma ya upasuaji kwa watoto ambao baadhi yao wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka nchini India.

“Pia nimefarijika kukuta kiwanda chako kipo hai na kinafanya kazi nzuri ya kusalisha magodoro bora. Nakupongeza kwa kutekeleza wito wetu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa kuajiri Watanzania 147 kati ya  watumishi 150 walioajiriwa kiwandani hapa,” alisema.

Bw. Gulamali alisema anatarajia kuwekeza katika ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti kitakachogharimu sh. bilioni nne hivyo kitaongeza fursa ya ajira kwa Watanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...