*Kiwanja chauzwa kwa sh. milioni 240 lakini zilizoingia CDA ni milioni 6 tu
*Ahimiza kasi ya upimaji viwanja, asema waliolipa nusu wasinyang’anywe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Bw. Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja kilichouzwa na CDA kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia ofisini ni sh. milioni 6 tu. 
“Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ninataka ufuatilie mauzo ya kiwanja namba 26 block AA eneo la Kikuyu East ambacho kimeuzwa kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia CDA ni sh. milioni 6 tu. Nataka kujua nani ameingiza milioni 6 na nani kachukua hizo sh. milioni 234,” amesema. 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Oktoba 6, 2016) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma. 
Bila kutoa ufafanuzi zaidi, Waziri Mkuu amesema eneo hilo lilipaswa kuwa na kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo. 
Pia amemwagiza Katibu Mkuu huyo afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo la CDA ambalo wamepangishwa taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai kuwa mhusika alipewa bure na sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha juu. 
Waziri Mkuu amewaonya watumishi hao pamoja na viongozi wao waache tabia ya kushirikiana na madalali kuuza viwanja na akawataka wachape kazi wakijielekeza na kasi ya Serikali ya kuhamia Dodoma. 
“Tabia ya watumishi kushirikiana na madalali kuuza ardhi sasa basi. Hata hivyo, nimefarijika kukuta mmeanza kuweka mfumo wa kielektoniki katika baadhi ya huduma. Ni lazima mauzo ya viwanja sasa hivi yafanyike kwa njia ya kieletroniki, madalali hawana nafasi,” amesisitiza. 
Ameutaka uongozi wa CDA uongeze kasi ya upimaji viwanja kwa sababu mahitaji ni makubwa lakini akaonya kuwa wakati zoezi hilo likifanyika, wananchi walionunua viwanja na bado hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa kigezo cha kutaka kuwauzia wengine.
 “Mimi nataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia msitumie fursa hii kuwanyang’anya watu wenye umiliki halali eti kwa sababu Serikali inataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke,” amesema. 
“Kama mtu amepewa offer au hati yake asinyang’anywe hata kama amelipia nusu asinyang’anywe. Ahimizwe kumalizia hilo deni na ninyi kazi yenu ni kupima viwanja vingine,” amesisitiza. 
“Natambua mnayo benki ya viwanja, lakini inabidi muongeze idadi ya viwanja vingi zaidi. Tumeita wawekezaji waje kujenga nyumba za kuishi watumishi, mahoteli na viwanda na maeneo yote haya inabidi yatengwe rasmi,” amesema.

Amesema jumla ya viwanja 70,000 vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973. Amesema kama wataendelea na kasi hiyo wakati mahitaji yameongezeka, itawachukua zaidi ya miaka 40 kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000 ambavyo vinatarajiwa kuanza kupimwa hivi karibuni. 
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Eng. Paskasi Muragili amesema usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika na kwamba wana lengo la kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni 2017. 
Waziri Mkuu alitembelea Ofisi ya CDA na kukagua mfumo wa utunzaji mafaili wa zamani pamoja na uhamishaji wa taarifa za wenye viwanja kwenye mfumo wa kompyuta. Pia alikagua mifumo ya uuzaji viwanja kwa njia ya mtandao ambayo hata hivyo bado haijakamilika. 
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amepokea mchango wa zaidi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Wilaya wa Kongwa, Bw. Deogratius Ndejembi zikiwa ni kwa ajili ya wakazi wa mkoa wa Kagera walioathirika kwa tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu. 
Pia Waziri Mkuu amepokea mchango mwingine wa zaidi ya sh. milioni tano kutoka kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiasha wa Manispaa ya Dodoma wakiwemo wamiliki wa hoteli, nyumba za kulala wageni, waendesha bodaboda na madereva wa daladala. 
Akipokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wafanyabiashara hao na kuwahakikishia kwamba fedha hizo zitapelekwa mkoani Kagera na kuwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, OKTOBA 6, 2016
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Mamalaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma leo.
 Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati  alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma leo
Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati  alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma leo.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...