Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekutana na Balozi Mpya wa Canada nchini, Ian Myles kuzungumzia masuala mbalimbali ya uendelezaji wa Sekta za Nishati na Madini nchini.

Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza kwa Balozi huyo kufika wizarani tangu alipowasili nchini mwezi Agosti mwaka huu ili kuiwakilisha nchi ya Canada.

Awali Balozi Myles alimweleza Profesa Muhongo kuwa nchi hiyo imeshiriki katika shughuli mbalimbali za uendelezaji wa sekta za Nishati na Madini nchini.

Mathalani, kupitia Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA) nchi hiyo ilikuwa ikitoa fedha kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA) katika mwaka wa Fedha wa 2012/2013 hadi 2015/2016 ili kuuwezesha Wakala huo kufanya shughuli zake za ukaguzi kwa ufanisi pamoja na kujengewa uwezo kupitia mafunzo ambapo jumla ya fedha zilizotolewa ni Dola za Canada 2500.

"Katika Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta (TEITI), Canada ilishiriki katika kusaidia mchakato wa maandalizi ya kupata Sheria ya kuongoza Tasnia ambayo ilipitishwa na Bunge mwaka 2015. Pia tunawajengea uwezo wataalam ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi," alisema Balozi Myles

Aidha, alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele na Serikali ya Canada katika masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa misaada ya kifedha.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa na Balozi Mpya wa Canada nchini, Ian Myles (kushoto) na Kamishna wa Biashara katika Ubalozi huo, Anita Kundy mara baada ya kumaliza kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam.
Balozi Mpya wa Canada nchini, Ian Myles akitia saini katika kitabu cha Wageni mara baada ya kumaliza mazungumzo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kamishna wa Biashara katika Ubalozi huo, Anita Kundy .
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika kikao na Balozi Mpya wa Canada nchini, Ian Myles (kulia kwa Waziri ) na Kamishna wa Biashara katika Ubalozi huo, Anita Kundy (kulia kwa Balozi). Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watendaji wa Wizara na Taasisi zake. Kushoto kwa Waziri ni Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga na wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Julius Sarota. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...