Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi,  Mhe.  William Ole Nasha akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika Bunge la 11 Mjini Dodoma.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhamishia Bodi ya Pamba katika Mkoa wa Mwanza kabla ya Novemba 10 mwaka huu ili kuhakikisha wakulima wa pamba waliopo katika mkoa huo wanapata huduma zilizo bora kwa ukaribu na haraka.

Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe.  William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bukombe Mhe. Doto Biteko lililohoji juu ya hatua ya Serikali kwa wakulima walioathirika na pembejeo zilizotolewa ambazo hazikuwa na ubora pamoja na kuhamishia Bodi ya Pamba katika mkoa huo.

”ili kuwafikia kirahisi wakulima wa pamba waliopo mkoani Mwanza, Wizara imeamua kuhamishia Bodi hiyo katika mkoa huo na kwa taarifa zilizopo Bodi hiyo inatakiwa kuhama haraka iwezekanavyo kabla ya Novemba 10 mwaka huu”, alisema Mhe.Ole Nasha.

Kwa upande wa matatizo ya pembejeo, Mhe. Ole Nasha amesema kuwa Serikali tayari ina taarifa kuhusu tatizo lililowapata wakulima wa pamba katika maeneo mbalimbali kwa kusambaziwa viuatilifu pamoja na mbegu ambazo hazikuwa na ubora unaotakiwa hivyo kuathiri wakulima nchini.

“Serikali iliiagiza Tropical Pesticides Research Institute (TPRI) kufanya uchunguzi wa malalamiko ya wakulima ambao ulibaini kuwa viuatilifu hivyo vilikuwa na utendaji hafifu hivyo Serikali itaanza kuzalisha mbegu bora za pamba za UK08 ili kuhakikisha tatizo hili halijirudii tena”, alisema Mhe. Ole Nasha.

Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa kufuatia changamoto hizo za uotaji wa mbegu, Serikali iliamua kufanya majaribio ya utoaji wa mbegu ambazo zilikuwa zikisambazwa hapo awali bila kujua ufanisi katika uotaji wake.

Amethibitisha kuwa, matokeo ya jaribio hilo yamewezesha kutoa maelekezo kuhusu aina za mbegu za pamba zenye sifa za msingi ambazo zitasambazwa kwa wakulima katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...