Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma hivi karibuni imeanza mchakato wa kuanzisha Redio ya jamii (community radio )itakayorusha matangazo yake ndani ya wilaya hiyo ya Namtumbo.
Ofisa habari wa wilaya ya Namtumbo Yeremias Ngerangera alisema kuwa mchakato wa kuanzisha Redio hiyo ya jamii unaendelea vizuri ambapo kwa hatua ya awali kamati ya kuanzisha Redio iliundwa na tayari kamati hiyo imeanza kazi yake .
Bwana Ngerangera alitaja idara zilizopo kwenye kamati hiyo ni idara ya mipango,idara ya utawala,idara ya maendeleo ya jamii, idara ya afya ,idara ya mazingira pamoja na kukihusisha kitengo cha sheria na usalama .
Aidha bwana Ngerangera alibainisha sababu za halmashauri hiyo kuanzisha Redio hiyo ni pamoja na kurahisisha mawasiliano kati ya uongozi wa halmashauri hiyo na wananchi wake juu ya maagizo mbalimbali ambayo halmashauri inawataka wananchi wake kufanya.
Pia redio hiyo itatumika pia kuelimisha jamii ya Namtumbo kuhusiana na kilimo bora ,umuhimu wa utunzaji wa mazingira ,umuhimu wa kuwapatia watoto elimu,umuhimu wa kuwa na afya bora pamoja na kuwatangazia wananchi mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Kaimu afisa mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Gwakisa Mwaseba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kuanzisha Redio hiyo alisema kuwa zaidi ya milioni 103,400,000 zinahitajika ili kukamilisha zoezi la kuanzisha redio hiyo.
Bwana Gwakisa aliwataka wadau kutoka sehemu mbalimbali katika nchi hii ,wazaliwa wa wilaya ya Namtumbo na wenye mapenzi mema na Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kushirikiana katika kuhakikisha redio hiyo inaanzishwa .
Pamoja na mambo mengine aliwaomba wadau kuchangia uanzishaji wa redio hiyo kwa kuwa redio hiyo itakuwa na umuhimu mkubwa kwa Halmashauri yetu ya Namtumbo na wilaya nzima ya Namtumbo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Christopher Kilungu aliitaka kamati hiyo ya kuanzisha Redio kufanya mikutano yao na kuwasilisha mapendekezo ya kamati yao kwenye uongozi wa Halmashauri kwa lengo la kujiridhisha na kuyajadili mapendekezo hayo .
Pamoja na mambo mengine mkurugenzi huyo aliitaka kamati hiyo kufanya kazi yake vizuri na kuhakikisha Redio hiyo ya Halmashauri inaanzishwa kwa madai kuwa Redio hiyo itakuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi wa Namtumbo na Halmashauri yao.
Wananchi wa wilaya ya Namtumbo walipoelezwa kupitia mikutano ya Hadhara kuhusiana na Hatua ya kuanzisha Redio hiyo walifurahishwa na hatua hiyo kwa madai ya kuwasaidia katika kutoa maoni yao kupitia kadi za salamu zitakazosomwa kwenye Radio hiyo.
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina jumla ya Tarafa Tatu, kata ishirini na moja na vijiji sabini na moja ambapo ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,375.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...