Na Mathias Canal, Bukoba
Kukosekana kwa huduma bora na msingi kwa wazee nchini imetajwa kuwa changamoto kubwa kwa Wazee waishio katika kambi mbalimbali za serikali na zile za binafsi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya METDO Tanzania (Mining and Environmental Transformation for Development  Organization) Bw Ashraf Omary wakati akikabidhi mahitaji kwa wazee wa kituo cha KIILIMA kilichopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

Bw Omary alisema kuwa Asasi hiyo yenye usajili No. ooNGO/08317 inajishughulisha na kutoa Elimu ya Mazingira kwa wananchi wanozunguka migodi pamoja na wafanyakazi wa migodini ambapo pia imejikita kuwasaidia wazee waishio katika kambi mbalimbali nchini katika huduma za kuwapatia mahitaji ya msingi ya kila siku kama vile (Chakula, na Mavazi) sambamba na kutoa huduma ya upimaji wa afya zao kupitia wataalamu wa tiba na kuwapatia dawa kwa ajili ya matibabu ya magonjwa mbalimbali.

Alisema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la wazee kutopatiwa huduma bora ikiwemo chakula na matibabu jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia wazee wengi kufariki pasina huduma yoyote ya kitabibu sambamba na kukosa Lishe Bora.

Bw Omary ameushukuru uongozi wa kampuni ya ZONGII PUMBLING LTD ya Jijini Mwanza kwa kushirikiana na METDO Tanzania kufanikisha kupatikana mahitaji mbalimbali kwa ajili ya wazee wa kambi ya KIILIMA sambamba na kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa ushirikiano ulioonyesha ikiwa ni pamoja na kuruhusu madaktari kwa ajili ya kwenda kuwapima afya wazee hao.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa METDO Tanzania Bw Hussein Sungura amebainisha kadhia zinazowakumba wazee katika kituo cha KIILIMA sambamba na vituo vingine nchini kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma za usafiri ili kurahisisha wazee kufikishwa haraka hospitalini pindi wauguapo, Ufinyu wa Bajeti, Ukosefu wa vitendea kazi kama vile vifaa vya usafi na ucheleweshaji wa Ruzuku ya serikali.

Sungura alisema kuwa Mpaka sasa Asasi hii ya METDO Tanzania imesaidia katika maeneo mbalimbali ikiwemo tukio la Agosti 13, 2016 la kumuenzi Mwl Julius Kambarage Nyerere katika Makao ya wazee wasiojiweza BUKUMBI Mwanza, Tukio la Octoba Mosi 2016 SIKU YA WAZEE DUNIANI katika wilaya ya Shinyanga ambapo jamii ilishirikishwa kutambua changamoto zilizopo katika kituo cha Wakoma na Wazee wasiojiweza cha KOLANDOTO pamoja na Kituo cha Wakoma na  Wazee wasiojiweza cha NYABANGE BUTIAMA  na kuwa sehemu ya kuzitatua changamoto hizo.
Mratibu wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya METDO Tanzania  Mathias Canal akimkabidhi Kaimu Mkuu wa Kituo cha Wazee KIILIMA Bi Gladness Lwiza baadhi ya mahitaji kwa ajili ya wazee waishio kituoni hapo.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya METDO Tanzania (Mining and Environmental Transformation for Development  Organization) Bw Ashraf Omary akimsikiliza kwa makini mzee aliyelala kutokana na homa kali inayomsumbua
Pichani katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Salum Kijuu, Kushoto kwake ni Mathias Canal Mratibu wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya METDO Tanzania, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kagera Ndg Charles  Mafimbo, Kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni Hussein Sungura Meneja Mradi METDO Tanzania na Mkurugenzi wa METDO Tanzania Ndg Ashrafu Omary
Mkurugenzi wa METDO Tanzania Bw Ashraf Omary mwenye Jembe akimsaidia kazi Mzee Wilson Ziraimani, Mzee huyu alikuwa anafanya kazi za kilimo katika mashamba mbalimbali nchini, yeye ni mkazi wa Ngara na wakati akiwa mtoto alikuwa analelewa na Mama wa kambo.
Aliwasili katika kituo cha kulelea Wazee cha KIILIMA Mwaka 1986 hapo alipo anatambaa kwani alivunjika kiuno enzi za ujana wake baada ya kuanguka mtini wakati alipokuwa anakata kuni kwa ajili kupikia.

HABARI ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...