Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Dar es Salaam.

KAMANDA wa Polisi wa kikosi cha usalama Barabarani Mohammed Mpinga ametoa wito kwa madereva wote ikiwemo madereva wa Serikali na Mashirika ya Umma kuzingatia sheria za Usalama Barabarani.

Kamanda Mpinga ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya “Abiria paza sauti”inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe 28 Novemba, mwaka huu.

Kamanda Mpinga alisema kumekuwa tabia ya baadhi ya madereva hususani wa Serikali na mashirika ya umma ya kutofuata sheria za usalama barabarani kwa kuendesha magari kwa mwendokasi, na kuwaonya kuwa sheria ni msumeno na inapaswa kufuatwa na kila mtu.

“Kumekuwa na madereva hasa wa magari madogo kusafiri kwenda maeneo mbalimbali ya nchi huku wakiwa hawana uzoefu wa kuendesha umbali mrefu na hivyo kupelekea uvunjifu wa sheria za barabarani kwa kuendesha kwa mwendokasi na kusababisha ajali” alifafanua Kamanda Mpinga.

Akifafanua zaidi Kamanda alisema uzoefu unaonyesha kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka kumekuwa na ongezeko kubwa la magari barabarani, na hivyo kuwataka wananchi kuzingatia sheria za barabarani ili kuweza kupunguza ajali za barabarani.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani, Jackson Kalikumtima alisema lengo la kampeni ya Paza Sauti ni kuhamasisha ushiriki kamilifu wa wananchi katika kukabiliana na ajali kwa kuchukua hatua stahiki bila ya uwepo wa askari.

Pia alisema kuwa kampeni hiyo imelenga kubadili tabia na mtazamo wa madereva kuhusu usalama barabarani ili waendeshe kwa kuzingatia sheria bila shuruti na kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu usalama barabarani ili watambue kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja.

Naye Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, (ASP), Deus Sokoni alisema mkakati wa kupunguza ajali barabarani katika kampeni hiyo  umelenga katika kutoa elimu kwa jamii ili kuona suala la usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja na si jukumu la Polisi pekee.

“hakuna asiyetumia barabara duniani, hatutaki ajali tunataka kuishi salama, hivyo kila abiria anawajibu wa kutunza na kutii sheria za barabarani “ aliongeza Mwanasheria huyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria Taifa (CHAKUA), Hassan Mhanjama aliwataka abiria wote nchini hususani wanaotajaria kusafiri mwishoni mwa mwaka kuwasiliana na Mamlaka ya Usafirishaji SUMATRA pindi watakapopandishiwa nauli mbali na taratibu zilizopo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...