Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Wafanyabiashara mkoani hapa wametakiwa kuchangamkia fursa mbali mbali pamoja na kurasimisha biashara zao ili kutambuliwa  na serikali na taasisi za fedha.
Hatua hiyo, imesemekana, itawasaidia kuingia katika ushindani wa kutafuta masoko na kukua kimitaji.
 
Ushauri huo umetolewa jana wakati wa ufunguzi wa semina ya siku tano kwa wafanyabiashara mkoani Mbeya jana na Katibu Tawala mkoa wa Mbeya, Bi. Mariam Mtunguja.
 
Mafunzo hayo yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  (BRELA),  yanalenga kuwajengea uwezo wa namna ya kurasimisha biashara zao na kuzisajili ili kutambuliwa na mamlaka zinazohusika.
 
“Hii ni fursa kwenu wafanyabiashara muitumie vizuri,” alisema Bi. Mtunguja.
 
Alisema wafanyabiashara katika mkoa wake wana wajibu wa kusajili biashara na kuzirasimisha ili kufanya biashara kisasa na sio kwa mtindo wanaoutumia sasa wa kufanya biashara bila kutambuliwa.
 
“Nawapongeza sana Brela kwa hatua hii, kwa kweli mmetufanyia jambo kubwa katika mkoa wetu,” aliongeza.
 
Aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa wakishatambuliwa na taasisi za fedha na vyombo vingine ni rahisi kupiga hatua na kusisitiza kutekeleza ushauri watakaopata katika semina hiyo.
 
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Bw. Frank Kanyusi alisema suala la kusajili jina la biashara ni la lazima kwa mujibu wa sheria.
 
“Tumeshatoa maelekezo kwa wafanyabiashara wote nchini kusajili majina ya biashara zao,” alisema Kanyusi na kusisitiza kuwa sheria kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokaidi agizo hilo.  
 
Alisema serikali inapoteza mapato mengi kwa kutowatambua wafanyabiashara, hivyo ni wajibu wa kila mfanyabiashara kuisaidia serikali katika hilo.
 
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabishara wa mkoa wa Mbeya,  Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa mkoa huo, Bw. Emile Malinza  alisifu hatua ya wakala huo.
 
“Hii ni namna ya kutujenga kifikra na ni muhimu wafanyabiashara wa Mbeya wakalitambua hili,” alisema Malinza ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa TCCIA mkoani humo.
 
Alisema mkoa wa Mbeya una wafanyabiashara wengi, lakini hawatambuliki katika mamlaka husika, na kuongeza kuwa hii ni fursa kwao kujisali na kutambuliwa.
 Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Bi.Mariam Mtunguja, (kulia)  akisindikizwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( Brela) Bw. Frank Kanyus, (katikati), katika Ukumbi wa mikutano wa Benjamini Mkapa, ambapo alifungua mafunzo ya siku tano kwa wafanyabiashara wa mkoa huo, mafunzo yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  ( BRELA),  yanalenga kuwajengea uwezo wa namna ya kurasimisha  na kusajili biashara zao, (kushoto) ni Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Bunifu kutoka Brela, Bi. Loy Mhando.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( Brela) Bw. Frank Kanyus ( kushoto) akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya siku tano kwa wafanyabiashara wa Mkoa Mbeya, mafunzo yanayotolewa na  BRELA, yanalenga kuwajengea uwezo wa namna ya kurasimisha  na kusajili biashara zao, (katikati) ni Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Bi.Mariam Mtunguja, (kulia) ni Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Bunifu kutoka Brela, Bi. Loy Mhando.
Baadhi ya wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya wakisikiliza kwa makini mafunzo katika ukumbi wa Benjamini Mkapa, mafunzo hayo ya siku tano yalifunguliwa na Katibu Tawala Mkoa wa huo Bi.Mariam Mtunguja,  mafunzo yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  ( BRELA),  yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kurasimisha  na kusajili biashara zao

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...