Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea kutoka Tanzania hivi karibuni amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mbegu CAJ ya Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea Hakilimiki la Kimataifa (The International Union for the Protection of New varieties of Plants - UPOV) 

Wanachama wa Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (UPOV) mwishoni mwa mwezi Oktoba walikutana Jijini Geneva, Uswisi ambapo pamoja na ajenda zingine, walilifanya uchaguzi wa viongozi wa Shirika hili akiwemo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Utawala (Legal and Administrative Committee - CAJ). Hii ndiyo Kamati ya juu inayolishauri Baraza la UPOV kuhusu masuala yote ya kitaalamu na kisheria. Kwa kawaida pamoja na kazi ya kumsaidia Mwenyekiti wake, Makamu Mwenyekiti huandaliwa kuwa Mwenyekiti mara tu kipindi cha Mwenyekiti wa CAJ kinapoisha. 
Katika uchaguzi huo, Mwakilishi wa Tanzania kwenye Baraza la UPOV, Bwana Patrick Ngwediagi, alichaguliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CAJ. 
Bwana Ngwediagi ni Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (Tanzania Bara) na anao utaalamu na zoefu mkubwa katika masuala ya hakimiliki za mbegu, mfumo wa hakimiliki wa shirika la UPOV na tasnia ya mbegu kwa ujumla na pia ni mkufunzi wa wakufunzi (trainer of trainers) katika masuala ya hakimiliki za wagunduzi wa mbegu mpya kwa mujibu wa Mkataba wa UPOV wa mwaka 1991. 
Aidha, Bwana Ngwediagi alisimamia na kuratibu kwa weledi mkubwa mchakato mrefu wa kuiwezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwanachama wa UPOV. Mchakato huo ulihusisha kupitishwa kwa Azimio la Bunge kuhusu kuridhia Mkataba wa UPOV wa mwaka 1991 na kutungwa kwa sheria ya Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea kwa upande wa Tanzania Bara (2012) na Zanzibar (2014). Kuanzia tarehe 22 Novemba, 2015, Tanzania ni mwanachama wa 74 wa UPOV na kabla ya hapo ilikuwa Mwanachama Mwangalizi (Observer). 
Bwana Ngwediagi pia ni mbobezi wa masuala ya mbegu katika ngazi ya Kikanda na Kimataifa. Kwa sasa yeye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mbegu ya Afrika iitwayo, AfricaSeeds. Taasisi hiyo inaundwa na nchi wanachama (Inter-governmental organization) wa Umoja wa Afrika (AU). Africa Seeds ndiyo taasisi iliyopewa jukumu la kutekeleza na kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Africa Seed and Biotechnology Programme (ASBP) wa Umoja wa Afrika (AU). 
Kuchaguliwa kwa Bwana Ngwediagi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CAJ, pamoja na kuongeza heshima ya Tanzania kimataifa, nafasi hiyo pia itaitangaza Tanzania na hivyo kuongeza uwekezaji katika ugunduzi wa mbegu mpya, uzalishaji wa mbegu na kilimo kwa ujumla.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...