Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu leo tarehe 28 Novemba, 2016 wamekubaliana kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuboresha utendaji kazi wa reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA ili miradi hiyo miwili ilete manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi Tanzania na Zambia.

Marais hao wametangaza kuchukua hatua hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika muda mfupi baada viongozi hao kufanya mazungumzo rasmi ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku 3 ya Rais Lungu iliyoanza jana hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Magufuli.

Katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya redio, tevisheni na mitandao ya kijamii Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na kuzorota kwa utendaji kazi wa reli ya TAZARA ambao umeshuka kutoka usafirishaji wa tani 5,000,000 za mizigo mwaka 1976 hadi kufikia usafirishaji wa tani 128,000 kwa mwaka hivi sasa, huku utendaji kazi wa bomba la mafuta la TAZAMA nao ukiporomoka kutoka uwezo wake wa kusafirisha tani 1,100,000 za mafuta hadi kufikia tani 600,000 kwa mwaka hivi sasa.

Marais hao wamekubaliana kuwakutanisha wanasheria wakuu wa Serikali za nchi zote mbili haraka iwezekanavyo kwa lengo la kufanya marekebisho ya kisheria kwa maeneo yote yaliyoonesha kuwa kikwazo na pia kupanga upya menejimenti za TAZARA na TAZAMA ili ziweze kuendesha vyombo hivyo kibiashara na kwa manufaa yaliyokusudiwa wakati vilipoanzishwa na Waasisi wa mataifa haya mawili yaani Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia.

"Tumekubaliana ni lazima tubadilike na tubadilike kwa haraka, vikwazo vinavyotokana na sheria viondolewe na manejimenti ya TAZARA ipangwe upya, na mimi nataka kusema kwa uwazi, ukiwauliza TAZARA watakwambia tatizo ni mtaji lakini ukweli ni kwamba tatizo ni menejimenti, ingekuwa tatizo ni mtaji, ule uliokuwepo mwaka 1976 umekwenda wapi? maana sasa hivi TAZARA ina vichwa 14 tu vya kuendeshea treni na ina upungufu mkubwa wa mabehewa" amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Rais Lungu amesisitiza kuwa katika kuimarisha TAZARA wamekubaliana kuweka pembeni siasa na kuirejesha TAZARA katika hali yake ya kibiashara kwa kuhakikisha inafanya kazi ya kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo iendayo kusini mwa Tanzania na nchini Zambia. 
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia Edgar Lungu (aliyekaa) leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
  Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Lungu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri wa TanzaniaDkt. John Pombe Joseph Magufuli (aliyekaa) leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia wakisaini makubaliano ya kuwa na Mashauriano ya Kidiplomasia leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia wakionyesha mikataba ya makubaliano ya kuwa na Mashauriano ya Kidiplomasia iliyotiwa saini leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na mgeni wake Rais wa Zambia Edgar Lungu (mwenye tai nyekundu) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania na Zambia leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha zote na: Frank Shija – MAELEZO.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...