Na Mwandishi Wetu,Songwe

SERIKALI Mkoani Songwe imewataka wafanyabiashara mkoani humo, kubadilika kimtazamo kwa kuachana na biashara za uchuuzi ili kuingia katika ushindani wa kweli utakaoleta tija na kukuza uchumi wa mkoa na mtu mmoja mmoja.

Mkuu wa mkoa wa Songwe Captain Mstaafu Chiku Galawa alitoa changamoto hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya siku tano, yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA), mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo wafanya biashara namna ya kurasimisha na kusajili biashara zao.

“Mafunzo haya ni fursa kubwa, naomba itumieni na kuichukulia kama changamoto ya kubadilika,” alisema Captain Galawa.Alisema ujio wa Brela katika mkoa wake ni njia mojawapo ya mwanzo wa kuibua fursa na kuwajenga kifikra na kimtazamo wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakifanya bishara kimazoea.“Naomba mbadilike, Brela wametuletea kitu kipya kwetu ni lazima tuamke,” alisema,

Bi.Galawa, alisisitiza kua biashara nyingi zimekua zikifanywa kwa uchuuzi na kuongeza kua bila kua na mtazamo wa mbele ni vigumu kuendelea.“Sajili biashara yako irasimishe uanze kushindana, mmezoea vibiashara vidogo vidogo, havina tija kwenu,” alisisitiza.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) Frank Kanyus amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Songwe kwa jitihada zake za kuhamasisha wafanyabiashara wake ambao walijitokeza kwa wingi na kupewa elimu ya namna ya kusajili na kurasimisha majina ya biashara na kampuni zao.“Namshukuru kwa namna ya pekee mheshimiwa mkuu wa mkoa mama Galawa, ameleta hamasa kubwa,"alisema Kanyus.

Alisema namna wafanyabiashara wa Mkoa wa Songwe walivyojitokeza, imeonyesha ni namna gani Mkuu wa mkoa huyo alivyo na mwamko wa kuufanya mkoa wake ukue kimaendeleo kwa haraka kupitia wafanyabiashara na wawekezaji.“ Huu ni mfano wa kuigwa, wafanyabiashara wamekuja kwa wingi mbali na kupata mafunzo lakini wamesajili majina ya biashara zao,” aliongeza

Aidha Kanyus aliwashukuru wakuu wa Mikoa yote waliyopita na kutoa mafunzo, ikiwa ni pamoja na kusajili majina ya biashara, kuwa wameonyesha ushirikiano wa hali ya juu kwa Wakala huyo.“ Kwa kweli nawapongeza sana, wakuu wa mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Mbeya, kwa kutupokea vizuri,” aliongeza.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoani Songwe, Bw. Ditrick Mapunda amesema ujio wa Brela katika mkoa wake umesaidia kurahisisha zoezi ambalo lilikua likiwagharimu wafanyabiashara kwa kiasi kikubwa kwa kutumia muda mwingi.“ Hii ni neema kwetu, wafanyabiashara wamekua wakitumia muda mwingi na gharama kubwa kwenda Dar es Salaam kusajili majina ya Biashara,” alisema Mapunda.

BRELA ipo katika zoezi endelevu la kuhamasisha wafanyabiashara kurasimisha na kusajili majina ya biashara zao nchini nzima.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Captain Mstaafu Chiku Galawa ( kushoto) akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafanyabiashara na watendaji wa Mkoa wa Songwe wakati wa mafunzo ya siku tano, yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa leseni na Biashara ( BRELA), mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kurasimisha na kusajili biashara zao, (katikati) ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela Frank Kanyus (kulia) ,Msajili Msaidizi Mwandamizi wa Mampuni Bw. Noel Chani, mafunzo hayo yanakwenda sambamba na zoezi la usajili wa papo kwa papo wa majina ya biashara.
Baadhi ya wafanyabiashara na Watendaji wa Mkoa wa Songwe, wakimfuatilia kwa makini mtoa mada kutoka wakala wa usajili wa biashara na Leseni ( BRELA) hayupo pichani, wakati wa mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na Brela, mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kurasimisha na kusajili biashara zao, mafunzo hayo yanakwenda sambamba na zoezi la usajili wa papo kwa papo wa majina ya biashara.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Captain Mstaafu Chiku Galawa ( kulia) akiwa katiaka akizungumza jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) Frank Kanyus ( kushoto) muda mfupi mara baada ya kufungua mafunzo ya siku tano, yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa leseni na Biashara ( BRELA), mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kurasimisha na kusajili biashara zao, ( katikati) ni Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Songwe Bw. Ditrick Mapunda

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...