Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.

Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kujenga Mahakama 40 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuongeza ufanisi na kuharakisha hukumu za kesi katika ngazi mbalimbali nchini.

Kutokana na fedha itakayotumika kujenga mahakama, shilingi bilioni 36 zinatokana na Bajeti ya mwaka huu wa fedha wakati shilingi bilioni 12.3 zilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Hayo yamebainishwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iramba Mashariki Mhe. Allan Kiula aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya na uteuzi wa Mahakimu katika ngazi hiyo.

Waziri Mwakyembe amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Mahakama zinakuwepo kila wilaya ili kuwaondolea usumbufu wananchi, kurahisisha usikilizwaji wa kesi pamoja na kupunguza gharama kwa wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine kufuata Mahakama zilipo.“Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria na Kanuni inaeleza kuwa kila Mahakama ina mipaka yake hivyo hatuwezi kubadilisha mahakama ya mwanzo kutumika kama ya wilaya” amesema Dkt. Mwakyembe.

Ameongeza kuwa mpaka sasa bado kuna wilaya zinapata huduma ya Mahakama kupitia wilaya nyingine ambapo amewahakikishia Wabunge na wananchi kuwa Serikali itajenga mahakama 40 kwa mwaka huu wa fedha.

Akifafanua mgawanyiko wa Mahakama 40 zinazotarajiwa kujengwa nchini, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali itajenga Mahakama Kuu nne, Mahakama za mikoa sita, Mahakama za Wilaya 14 na Mahakama za Mwanzo 16 katika wilaya mbalimbali nchini.

Aidha, Mhe. Mwakyembe ametaja baadhi ya vigezo vinavyotumika kuanzisha Mahakama katika eneo lolote kuwa pamoja na uwepo wa hati ya kisheria ya kuwepo kwa wilaya, mkoa, kata na kijiji, umbali wa upatikanaji wa huduma za Mahakama, idadi ya wakazi wa eneo husika pamoja na uwepo wa huduma zingine za kipolisi na magereza.

Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hizo za kukosekana kwa mahakama katika maeneo ambayo yamekidhi vigezo ndiyo yaliyopelekea Serikali kujipanga kujenga Mahakama hizo ambapo ametoa rai kwa wananchi kuwa na subira wakati wakikusubiri kujengwa kwa Mahakama hizo. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...