Serikali ya Tanzania imeishukuru Jamhuri ya watu wa China kwa ushirikiano katika maeneo mbalimbali yanayolenga kuleta ustawi kijamii na kukuza uchumi.Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt. Adelhelm Meru ametoa shukrani hizo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ofisi ya masuala ya biashara na uchumi ya jimbo la Jiangsu la nchini China hapa nchini.

Mbali na kuushukuru uongozi wa jimbo la Jiangsu kwa hatua hiyo, Dr. Meru alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuinua uchumi wa viwanda na kusimamia mpango wa uwekezaji wa viwanda kutoka jimbo hilo la China kuja Tanzania.“Tunatambua kuwa jimbo la Jiangsu limeendelea sana kiviwanda, hivyo kufunguliwa kwa ofisi hii kutasaidia sana katika kuhamasisha maendeleo ya viwanda hapa nchini,” alisema Dkt. Meru ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

China ni moja ya wadau wakubwa wa maendeleo wa Tanzania katika masuala ya biashara na uwekezaji.Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kamishna wa Biashara wa Jimbo la Jiangsu, Bw. Zhao Jin alisema ofisi hiyo ni ya 17 duniani na ya pili kwa bara la Afrika.Ofisi hiyo imefunguliwa kwa ushirikiano kati ya idara ya biashara ya jimbo la Jiangsu, manispaa ya Changzhou na Jiangsu Overseas Group Corporation.Manispaa ya Changzhou ndiyo inayomiliki asilimia 51 ya kiwanda cha nguo cha urafiki, China Friendship Textile.

“Kiwanda cha Urafiki na reli ya TAZARA ni alama za urafiki wa enzi kati ya Tanzania na China,” alisema Katibu wa Chama cha Kikomunisti katika jimbo la Changzhou, Bw. Yan Li.Eneo jipya la viwanda lijulikanalo kama "Jiangsu-Shinyanga Agricultural Industrial Zone” lililowekezwa na Jiangsu Overseas Group Corporation hapa nchini ndio uwekezaji mkubwa unaotaka kutekelezwa na jimbo la Jiangsu hapa nchini.Uwekezaji katika eneo hilo utafikia Dola za Kimarekani milioni 200.

Ofisi ya biashara na uchumi ya Jiangsu hapa Tanzania itashughulika pamoja na mambo mengine, kuimarisha hadhi ya jimbo hilo hapa nchini; kuhamasisha uwekezaji wa viwanda na kuimarisha njia za biashara kati ya nchi hizo mbili.Pia, ofisi hiyo itashirikiana na ubalozi wa China hapa nchini kufanya tafiti za ushirikiano zaidi katika maeneo ya uchumi na biashara.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Bw. Yan Li, Muwakilishi wa masuala ya Uchumi na Biashara wa China hapa Tanzania, Bw. Lin Zhiyong na Mwenyekiti wa CCM mkoani Singida, Bi. Martha Mlata.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji,Dkt.Adelhelm Meru (katikati)akipiga makofi muda mfupi)) baada ya kuzindua Ofisi ya uwakilishi wa biashara na Uchumi wa Jimbo la Jiangsu la China hapa nchini (Dar es Salaam) juzi. Wengine ni wakilishi wa jimbo hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...