Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunngano wa Tanzania Bi Samia Suluhu amewasihi viongozi wa serikali na wananchi kutumia ndege za Shirika la Ndege Tanzania(ATC) ili kudumisha uzalendo na kuchangia pato la shirika hilo kwa lengo la kuhimili ushindani na kukuza uchumi wa nchi.

Ametoa rai hiyo jijini Dar es salaam alipopewa hati ya kusafiria kupitia ndege za shirika hilo wakati akisafiri na ujumbe wake kuelekea mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi.“Napenda kutoa wito kwa viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla kutumia ndege zetu ili shirika letu lifanye kazi vizuri zaidi, kufanya hivi kutaongeza pato na kukuza uchumi wa nchi ”, amesema Makamu wa Rais.

Ametanabaisha kuwa kwa kutumia ndege za Shirika la ATC kwa safari za ndani Serikali itaokoa fedha nyingi zinazotumika kwa kukodi ndege za mashirika binafsi.“Mimi na ujumbe tumeamua kusafiri na ndege za shirika la ndege Tanzania kutokana na kubana matumizi, gharama tuliyotumia kwa safari hii ni shilingi Milioni saba na laki sita ambapo tungekodi ndege binafsi tungetumia milioni arobaini”, amefafanua Makamu wa Rais.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amempongeza Makamu huyo kwa kitendo cha uzalendo alichokionyesha na kutaka viongozi wengine wa Serikali na wananchi kwa ujumla kuiga mfano huo ili kuliinua shirika hilo na kuongeza uchumi.

“Nampongeza Makamu wa Rais kwa kuamua kutumia ndege za Shirika hili kwa safari za ndani, kitendo hiki kimeonesha nia ya dhati ya serikali ya kulifufua shirika hili, naomba wananchi nao waendelee kutumia ndege za shirika hili katika safari zao za ndani kama alivyofanya Makamu wa Rais”, amesema Waziri Mbarawa.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu akionyesha mfano wa hati ya safari ya kuelekea Mwanza kupitia Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), kushoto kwake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu akiongea na waandishi wa habari kabla ya kufanya ziara ya kikazimkoani Mwanza kupitia Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), leo jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipokea maoni kutoka kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa anga katika uwanja wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) wakati alipokagua utoaji wa huduma uwanjani hapo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipokea maoni kutoka kwa wasafiri wanaotumia usafiri waa anga katika uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere wakati alipotembelea kukagua huduma zitolewazo uwanjani hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...