Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepewa semina kuhusu Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya (EPA) ili wapate uelewa na hatimaye kuishauri Serikali juu ya suala hilo.
Semina hiyo imetolewa kwa Wabunge leo mjini Dodoma na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Saalam akiwemo Prof. Palamagamba Kabudi, Dkt. Ng’waza Kamata na Dkt. John Jingu pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda. 
Akifungua semina hiyo, Spika Mhe. Job Ndugai amesema kuwa anatambua umuhimu wa mkataba huo ni vema Wabunge watumie fursa ya semina hiyo ili watakapofika kwenye mjadala wenyewe ndani ya Bunge wawe na uelewa mpana kwa manufaa ya nchi.
“Natambua kwamba majadiliano haya yamefanyika sana hasa katika vikao vya Bunge lililopita, lakini kwa kuwa wabunge wengi ni wapya tumeona kuna umuhimu wa kuandaa Semina hii ili tuweze kupata elimu na kuongeza uelewa wa jambo hili kabla ya kuujadili rasmi ndani ya Bunge letu”, alisema Mhe. Ndugai.
Ameongeza kuwa semina hii pia itawapa wabunge nafasi ya kuuliza maswali na kufanya majadiliano ya jumla ili kupata ufafanuzi wa kina juu ya mambo mbalimbali yanayohusu mkataba huo, hiyo yote ikiwa ni njia ya kuwaelimisha ili siku ya majadiliano rasmi watoe mapendekezo yatakayoleta tija na manufaa kwa nchi yetu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda alipokuwa akiwasilisha mada juu ya chimbuko, mustakabali na uchambuzi wa EPA amesema hiyo ni namna bora ya kuwashirikisha na kuwapa uelewa Wabunge ili waweze kujadili mkataba huo kwa manufaa ya taifa. 
Nao wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamewashauri wabunge kutumia semina hiyo kama muongozo utakaowawezesha kuboresha mjadala wao wakati wa kutoa michango yao ndani ya Bunge ili waweze kutoa majibu sahihi siku ya kuujadili mkataba huo.
Mswada huo unatarajiwa kuwasililishwa Bungeni Novemba 10 mwaka huu ambapo mjadala huo utapelekea kuishauri Serikali kuhusu hatma ya mkataba huo.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai (kulia kwake) na wabunge wengine wakimsikiliza Profesa Paramgamba Kabudi, Mhadhiri  wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (kulia) wakati alipotoa mada kuhusu Mkataba wa EPA kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma Novemba 6, 2016. 
Profesa Paramgamba Kabudi, Mhadhiri  wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (kulia) akiendelea kutoa  mada kuhusu Mkataba wa EPA kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma Novemba 6, 2016. (Picha na Ofifi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...