WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya wabunge,
viongozi wa kitaifa na watumishi wa Ofisi ya Bunge kuuaga mwili wa Spika
Mstaafu, Samwel Sitta.
Bw. Sitta alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 7 katika
hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.Akizungumza wakati wa kuuaga mwili huo Bungeni mjini
Dodoma leo (Ijumaa, Novemba 11, 2016), Waziri Mkuu ametoa pole kwa Spika wa
Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, mke wa marehemu Mheshimiwa Magreth Sitta, mama wa
marehemu Hajat Zuena Fundikila na familia ya marehemu na wabunge wote.
“Nitumie fursa hii pia kukupa pole Mheshimiwa Spika kwa pigo
ambalo Bunge lako tukufu imelipata kwa kumpoteza mmoja wa viongozi mahiri wa
Bunge hili katika historia ya nchi yetu. Msiba uliotupata wa Spika Mstaafu wa Bunge la
Tisa (2005-2010) na Mbunge Mstaafu wa jimbo la Urambo mkoani Tabora ni mzito.”
Amesema Bw.
Sitta alikuwa mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
“Serikali imepokea taarifa za msiba huu kwa mshtuko mkubwa. Historia ya
Mzee Sitta ni pana sana. Tunatambua utumishi uliotukuka katika nyadhifa
mbalimbali alizozitumikia. Tutamkumbuka kwa utumishi wake,” amesema.
Waziri Mkuu
ameongeza kuwa: “Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu kila mtu kwa imani yake ili
tuweze kufikia japo mema machache aliyoyatenda katika enzi za uhai wake.”
Enzi za uhai
wake Mhe. Sitta alibahatika kufanya kazi na Marais wa awamu nne zilizopita
tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa mbunge
kwa miaka 30.
Nyadhifa
nyingine alizowahi kushika ni pamoja na Mkuu wa Mikoa ya Iringa na Kilimanjaro,
Waziri wa Ujenzi, Waziri anayesimamia Ustawishaji Makao Makuu, Waziri wa Katiba
na Sheria, Waziri wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
Mwili wa Spika Mstaafu, Samuel Sitta ukiingizwa bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
1A2358 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye jeneza la Spika Mstaafu Samwel Sitta, bungeni mjini Dodoma Novemba 11, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa Spika Mstaafu, Samuel Sitta, bungeni mjini Dodoma, Novemba 11, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
MOLA akupumzishe palipo pema peponi Marehemu Spika Mstaafu Mh. Samwel John Sitta. Wewe umetangulia nasi sote umauti ndio maishilizio yetu. Pumzika kwa amani pema peponi Marehem Mh. Spika Mstaafu John Samwel Sitta - AMEN.
ReplyDelete