Pichani ni Marehemu Hadija Bint Kamba enzi za uhai wake akiwa na Mzee Tamba katika moja ya hafla za CCM jijini Dar es salaam. 


 MAKALA  KWA HISANI YA SAIGON GROUP
Binti Kamba mwenye urefu wa wastani,  mweusi mwenye umbo lililosadifu Unyamwezi. Asili yake ni Tabora ndipo alipotokea Baba yake na Kigoma ndipo wazazi wa Mama yake walipotokea.


Ni kama ilivyo kwa familia ya Sykes, Bint Kamba alitoka katika familia mashuhuri jijini Dar es salaam katika miaka ya 1950s. Aliingia katika harakati za ukombozi akiwa bint mdogo mwenye malengo tofauti kabisa na yakipekee sana. Pamoja na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukoloni tena akiuza roho kwani alikuwa ni Bint pekee wa kiafrika aliyeweza kujichanganya na wazungu, hivyo aliweza kupata siri nyingi za wakoloni na kuwasaidia wapigania uhuru wasikamatwe na wakati mwingine wasidhurike. Alifanya kazi hii kwa siri kubwa sana, kiasi kwamba hakuwa akijulikana sana kwa watu hasa wanaharakati..alikuwa mtu mwenye uwezo wa kipekee wa kutunza siri.

Mwaka 1955 akiwa na Bibi Titi na Bint Maftah walishirikiana kuunda Baraza la Wanawake Tanganyika ikiwa ni kikundi ndani ya TANU kilichokuwa kikitoa ushawishi kwa akina mama kuiunga mkono TANU.

Mwaka 1961 wakati wa Uhuru, Bint Kamba alikuwa ni mmoja wa timu iliyoundwa kubuni nembo ya Taifa (maarufu kama nembo ya Ikulu ama nembo ya "Adamu na Hawa" ambayo mpaka sasa imeendelea kuwa alama kuu ya Taifa {baadhi ya waandishi wanamtaja kuwa yule mwanamke anayeonekana kwenye nembo hiyo ndiye Bint Kamba).

Novemba 2 ya Mwaka 1962 Mwalimu Nyerere alipotangaza kuunda Umoja wa Wanawake wa Tanganyika  (UWT) Bint Kamba alikuwa ndio mpanga mikakati na mfumo wa uongozi wa UWT.

Pamoja na kushiriki katika mapambano ya kudai uhuru akiwa msiri mkubwa wa Mwalimu Nyerere, Bint Kamba hakuwahi kushika nafasi yeyote ya kisiasa kwa kugombea ama kuteuliwa. Baada tu ya nchi kupata uhuru Bint Kamba alieleza kuwa LENGO lake limetimia na kwamba haitaji CHEO chochote.

Mwaka 1985 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Mwalimu Nyerere akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Pamoja na Baraza la Wazee wa Dar es salaam juu ya kung'atuka alimtaja mtu mmoja ambaye ni wa kipekee aliyeyashangaza maisha yake ya uongozi. Alimtaja Hadija Bint Kamba kuwa ni mwanaMAMA na MPAMBANAJI wa kipekee aliyeshiriki mapambano ya uhuru bila tamaa ya cheo. Mwalimu Nyerere alisema kuwa amekaa ikulu kwa miaka 25 na kila alipotaka kumteua, Hadija Bint Kamba aliendelea kubaki na msimamo wake kuwa HAKUPIGANIA CHEO bali alipigania HAKI na USAWA...alitaka kuona Mwafrika anathaminiwa katika nchi yake na kwamba ametimiza LENGO hilo.

Tangu Mwaka huo wa 1985, Mwalimu alimtangaza Bint Kamba kuwa ni Shujaa asiyevaa Nishani, na tangu wakati huo alishirikia vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mikutano Mikuu yote akiwa ni mwalikwa mpaka pale umri ulipokuwa mkubwa na kumfanya ashindwe kuhudhuria vikao na mikutano hiyo.

BIBI HADIJA BINT KAMBA amefariki  tarehe 30/11/2016 akiwa ni miongoni wa waasisi waliobahatika kuishi kwa muda mrefu katika nchi huru ya TANZANIA. Bint Kamba amezikwa mchana wa jana  tarehe 1 Desemba 2016 katika makaburi ya Kisutu yaliyopo jijini Dar es salaam.

Amekufa bila CHEO lakini amezikwa kwa heshima ya KIONGOZI wa kitaifa, kwa msafara wa Magari ya askari na viongozi wa Chama na Serikali kutoka mtaani kwake mtaa wenye jina lake Bint Kamba street Ilala Bungoni mpaka Kisutu. Maraisi wastaafu, Katibu Mkuu wa Chama, Naibu Katibu mkuu na Viongozi  wengine wa Chama wakiongoza jeneza lenye mwili wake.Amekufa bila UTAJIRI lakini amezikwa kwa HADHI ya Bilionea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. MUNGU AMPUMZISHE KWA AMANI MAMA YETU, MPIGANIA UHURU ALIYETUACHIA CHA KUJIFUNZA.....THAMANI YA MTU NI UTU SI KITU

    ReplyDelete
  2. Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiun. Mwenyeez Mungu amrahamu amughufirie kwa yote amlaze pema peponi AMEN.

    Naamini Taifa letu hili bado lina watu kadhaa au wengi ambao pia walikuwa ni waasisi either wa TANU au ASP (Kwa visiwani) na waliotowa mchango wao mkubwa mithili ya Marehemu Bi Khadija Binti Kamba, lakini bado hawatambuliki, kuonekana, kufahamika na hata kuujuwa umuhimu na hata mchango wao huo. Ni vyema tukawa tunawaenzi na kuwatambuwa kwa mapana tangu tungali nao hai na hata baada ya hapo ili waendelee kubaki kuwa ni kumbu kumbu na moja wapo ya historia ya nchi yetu na kwa vizazi vijavyo kwa umuhimu wa mchango wao katika Taifa letu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...