Na Lucas Mboje, Dar es Salaam
KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa(pichani) ameipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha
mchakato wa ununuzi wa magari 450 ya Jeshi hilo ambayo yanatarajiwa kupokelewa muda
wowote kuanzia sasa.
Kamishna Jenereli Malewa ameyasema hayo leo katika ufunguzi rasmi wa mkutano wa
wakuu wa magereza yote Tanzania Bara unaofanyika kwa siku moja katika Bwalo kuu la
Maafisa magereza, ukonga jijini Dar es Salaam.
Jenerali Malewa amesema kuwa upatikanaji wa magari hayo utapunguza tatizo kubwa la
uhaba wa magari kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na utawala pamoja uboreshaji wa
utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo.
“Nichukue nafasi hii kumshukuru kwa dhati Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja
na serikali yote kwa ujumla kwa namna inavyoshughulikia utafutaji wa ufumbuzi wa
changamoto tulizonazo,” alisema Jenerali Malewa.
Aidha kuhusu madeni ya Watumishi wa Jeshi hilo na wazabuni, Kamishna Jenerali Malewa
amesema serikali imetoa kiasi cha zaidi ya Bilioni 8 za pesa ya kitanzania kwa ajili ya kulipa
madeni hayo ambapo madeni yote yaliyokwisha kuhakikiwa tayari yameanza kulipwa na
wahusika wamekwishaanza kupata fedha wanazodai Jeshi hilo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Mhandisi Hamad Yusuph
Masauni akizunguza katika ufunguzi wa Mkutano huo ametoa rai kwa jeshi hilo kutumia
vyema fursa zilizopo katika katika maeneo mbalimbali ya jeshi hilo kwa kuanzisha na
kuimarisha viwanda vidovidogo vilivyopo ili kuongeza uzalishaji hivyo kuchangia pato la
taifa.
Masauni amesema kuwa Jeshi la Magereza linazo fursa nyingi sana za uzalishaji yakiwemo
maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo, miradi ya ufugaji na miradi mengineyo ya
kiuchumi.
“Nisisitiza kwamba wekeni mikakati yenye lengo la kuongeza uzalishaji katika maeneo yenu
kwani nataka kila mmoja wenu katika gereza alilopo aweke malengo ya kuongeza uzalishaji
kulingana na fursa zilizopo,” alisema Mhe. Masauni.
Mkutano huu wa Wakuu wa Magereza yote Tanzania Bara unajumuisha Maafisa
Waandamizi kutoka Makao Makuu ya Magereza na Wakuu wa vituo vya Magereza yote
nchini ambapo lengo kuu ni kujadiliana kwa kina hali halisi ya utendaji kazi magerezani na
kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuongeza tija na ufanisi. Kauli
mbiu ya mkutano huo ni JESHI LA MAGEREZA KATIKA JITIHADA ZA
KUFANIKISHA KUELEKEA TANZANIA YA UCHUMI WA VIWANDA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...