Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa anapenda kuendelea kufanya shughuli zinazosaidia kuleta maendeleo kwa watu na jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa  akizindua Taasisi yake ya Jakaya Kikwete (Jakaya Mrisho Kikwete Foundation)  alisema kuwa kwa muda mrefu amekua akipenda na kujihusisha na shughuli mbalimbali za maendeleo ya watu na hivyo Taasisi yake itamsaidia katika kufikia malengo yake.
“Nimetumia muda wangu kwa ajili ya maendeleo ya watu, baada ya shule, nilikitumikia Chama cha Mapinduzi(CCM), nilitumikia Jeshi na baadae Serikali, kwangu Taasisi hii imekuwa chombo kitakachonisaidia kuendeleza maono yangu na kutimiza ndoto zangu katika kuendelea kusaidia watu” alisema Dkt. Kikwete.

Akiizungumzia taasisi hiyo Kikwete alisema kuwa, Taasisi yake ina wajumbe 9 kutoka sehemu mbalimbali duniani wenye nyadhifa na heshima kubwa katika nchi zao.

Ameongeza kuwa Taasisi hiyo imejikita kusaidia jamii katika maeneo makubwa manne, maendeleo ya jamii  hasa katika kujikita kuondoa umaskini, mabadiliko ya hali ya nchi na kilimo  kwa wakulima wadogo.

Pia Taasisi hiyo imejikita katika huduma za afya, kutokomeza malaria na afya ya mama na mtoto.

Maeneo mengine ambayo Taasisi hiyo inajihusisha nayo ni  ni elimu kwa  vijana ili  kukuza vipaji vyao na kuwapa mafunzo kuhusu uongozi bora, usawa wa kijinsia na namna ambavyo Serikali inavyotoa huduma kwa wananchi.

Aidha, alisisitiza kuwa Taasisi yake itaisaidia Serikali, mashirika na Taasisi mbalimbali ili kushirikiana kuwaletea maendeleo watanzania na watu mbalimbali duniani.

Dkt. Kikwete amewataja Wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya Taasisi yake kuwa ni Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Profesa Rwekaza Mukandala Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Willium Mahalu Mhadhiri Mwandamizi  katika Chuo Kikuu cha Tabibu cha Bugando.

Wengine ni Balozi Mwanaidi Maajar aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Abubakar Bakhresa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Bakhresa, Genevieve Sangudi  Mtaalamu wa Masuala ya kibishara ya Kimataifa kutoka Marekani.

 Pia wapo Dato’ Sri  Idris Jala, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu nchini Malyasia,  Balozi Charles R. Stith aliyekuwa Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania pamoja na Dkt. Carlos Lopes ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taaisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).

Taasisi ya Maendeleo ya Jakaya Kikwete ilisajiliwa tarehe 17, Februari 2017, na hii ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini kukutana tangu kuanzishwa kwake. Imeandikwa na Immaculate Makilika- MAELEZO

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...