Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana amezikumbusha taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha zinaongeza uwezo wa madawati ya mikopo yaliyopo katika taasisi zao ili yaweze kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kutatua changamoto za utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Mkuu wa Mkoa huyo ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Machi 17, 2017) wakati akifungua mkutano wa kazi wa siku mbili kati ya watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na maafisa mikopo zaidi ya 100 kutoka taasisi za elimu ya juu nchini wanaokutana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Baadhi washiriki wa mkutano wa kazi kati ya HESLB na maafisa wasimamizi wa madawati ya mikopo ya elimu ya juu kutoka taasisi za elimu ya juu wakiwa katika picha ya pamoja mjini Dodoma leo (Alhamisi, Machi 16, 2017).

“Majukumu ya Bodi ni mazito na hivyo Bodi inahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali mkiwemo nyie maafisa mikopo mliopo vyuoni na mnaokutana na wanafunzi kila siku,” amesema Rugimbana katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi (Elimu) wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Gosbert Damazo.

Akizungumza katika mkutano huo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema Bodi yake inatambua mchango mkubwa unaotolewa na maafisa mikopo hao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waliopo katika taasisi mbalimbali.

“Maafisa hawa ndio wanaotuunganisha na wanafunzi katika utendaji kazi wetu wa kila siku, hivyo ni watu muhimu sana kwetu na tunathamini sana mchango wao na wa taasisi zao kwa ujumla,” amesema Bw. Badru.
Afisa Tawala Msaidizi (Elimu) wa Mkoa wa Dodoma Bw. Gosbert Damazo akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa kazi wa siku ya mbili kati ya HESLB na maafisa wasimamizi wa madawati ya mikopo ya elimu ya juu kutoka taasisi za elimu ya juu mjini Dodoma leo.

Kwa mujibu wa Bw. Badru, Bodi yake itatumia mkutano huo wa siku mbili kuwakumbusha maafisa hao wajibu wao katika kutunza kumbukumbu muhimu za wanufaika wa mikopo na majukumu yao muhimu ili kuongeza ufanisi na hivyo kupunguza malalamiko ya wadau wakiwemo wanafunzi wanaoufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo alikumbusha kuwa mwaka 2011, Serikali ilivielekeza vyuo vyote vya elimu ya juu nchini kuanzisha madawati ya mikopo ya elimu ya juu ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali.

“Tangu wakati huo (2011), kumekuwa na mafanikio makubwa katika utendaji wetu kutokana na kuongezeka kwa ufanisi. Hivi sasa, malalamiko kutoka kwa wanafunzi yamepungua sana kwa kuwa wana sehemu ya kuwasilisha hoja zao palepale chuoni …wito wangu kwao ni kuwa wayatumie madawati haya vizuri,” amesema Bw. Badru.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru akiongea katika mkutano kazi wa siku ya mbili kati ya HESLB na maafisa wasimamizi wa madawati ya mikopo ya elimu ya juu kutoka taasisi za elimu ya juu mjini Dodoma leo.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Taaluma) Prof. Lawrence Msoffe, ambaye alihudhuria hafla ya ufunguzi, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa utaisaidia Bodi kupata mrejesho kutoka kwa maafisa hao ambao ndio wanaosimamia masuala ya utoaji mikopo katika vyuo kila siku.

HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili, pamoja na mambo mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi watanzania wasio na uwezo na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...