Na Karama Kenyunko.
Upande wa Mashtaka katika kesi ya kujeruhi inayowakabili wabunge na makada wa Chadema wamefunga ushahidi wao. Katika kesi hiyo wabunge hao wanadaiwa kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando. 

Wakili wa Serikali, Flontina Sumawe amefunga ushahidi  wa upande wa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  upande wa mashtaka ulileta mashahidi wanne waliofika na kueleza kuwa washtakiwa walitenda kosa la kujeruhi.
Mahakama imewataka upande wa utetezi kuwasilisha hoja za kuomba washtakiwa wasionekane wana kesi ya kujibu Machi 21, wakati upande wa mashtaka utawasilisha majibu kinzani  Machi 28. Kesi hiyo itatajwa Aprili 5, mwaka huu. Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea, Halima Mdee, Kawe, Mbunge wa Jimbo Ukonga Mwita Waitara, diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema, kada wa chama hicho, Rafii Juma na Diwani wa Kata ya Saranga Kimara, Ephreim Kinyafu.

 Wanadaiwa kuwa Februari 27, 2016 katika Ukumbi wa Karimjee wilaya ya Ilala jiji la Dar es Salaam walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha. Akitoa ushahidi wake, Mmbando alieleza jinsi alivyovamiwa, kujeruhiwa na kupokonywa faili lililokuwa na ajenda na muongozo wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa jiji la Dar es Salaam uliopaswa kufanyika  Februari 27,2016. Alidai kuwa siku hiyo ya Februari 27, 2016 alipewa jukumu la kuusimamia uchaguzi huo wa Meya na Naibu Meya ambao ulipaswa kufanyika Karimjee.

Kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa ni Mwenyekiti  wa uchaguzi huo, wajumbe wote walifika , Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Salehe Yohana ambaye alikuwa Katibu alifungua uchaguzi  huo kwa idadi ya wajumbe ilikuwa inajitosheleza. Baada ya kikao kufunguliwa alipata taarifa ya zuio la mahakama na kuwatangazia wajumbe wote kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika. Baada ya uchaguzi huo kuahirishwa , wajumbe wa CCM walitoka nje lakini wajumbe wa vyama vingine wakiwamo Ukawa walimvamia wakisema aendeshe uchaguzi huo.

“Walinifuata mezani nilipokuwa nimekaa wakitaka niendelee na uchaguzi huo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alilivuta faili lililokuwa na muongozo wa uchaguzi huo na katika tukio hilo niliweza kuwafahamu walionivamia kwa wengine kwa majina, wengine kwa sura.”Alisisitiza kusema Mmbando wakati akitoa ushahidi wake.

Aliongeza kuwa kuna mwanamke mmoja alimkoa konzi kichwani na wengine wakimgonga gonga huku na kule Aliieleza mahakama watu wengine aliowatambua siku hiyo ya tukio kuwa ni Mbunge wa jimbo la Ubungo, Saed Kubenea akimwambia kuwa yeye ni Kibaraka wa CCM, hawawezi kuendesha serikali kama mali yao, akae aendeshe huo uchaguzi. Mbunge wa jimbo la Ukonga, Mwita Waitara yeye alikuwa akimsisitiza kuwa hakuna kuondoka hapa kaa uendeshe kikao.

Mheshimiwa Hakimu, walinikamata kwa nguvu nisitoke , wengine walinishika maziwa hadi sketi yangu iling’oka zipu na kwamba baada ya tukio hilo aliokolewa na askari wa jeshi lapolisi na wafanyakazi wa jiji  kupitia mlango wa nyuma   na hakujua kilichoendelea nyuma yake. “Katika tukio hili nilipata madhara, utu wangu nilidhalilika na mwili wangu ulivia damu”. Alimaliza kutoa ushahidi wake Mmbando.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...