Na Johary Kachwamba -TGDC

Wananchi wa Wilaya za Rungwe na Mbeya Vijijini pamoja na wadau wengine wa mradi wa jotoardhi wa Ngozi wametoa maoni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali ya msingi kabla ya zoezi la uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uvunaji mvuke wa kuzalisha umeme utakaotokana na nishati ya jotoardhi.

Wananchi walipata fursa ya kutoa maoni yao kati ya tarehe 6 hadi 11 Machi, 2017, wakati timu ya wataalamu wa Mazingira na Jamii kutoka Kampuni ya kuendeleza Jotoardhi Tanzania (TGDC) na TANESCO walipotembelea eneo la mradi, ikiwa ni matakwa ya kisheria ya kushirikisha wadau na jamii itakayopitiwa na mradi husika, wakati wa kufanya tathmini ya athari za mradi katika mazingira na jamii.

Maoni yao ilikuwa ni pamoja na kuiomba Serikali kusimamia taratibu za ajira wakati wa zoezi la uchorongaji visima vya jotoardhi, akizungumza Ndugu Yohana Julius wa Kata ya Swaya Vijijini alisema “wanaomba ajira zisizohitaji ujuzi wapatiwe wakazi wa eneo la mradi ili wanufaike moja kwa moja kwa kujiongezea kipato”

Bibi Mary Gwamaka alisema “wanaomba mradi huu usiwaache nyuma wakina mama, kwani wanao uwezo wa kufanya kazi mbalimbali, hivyo wanaomba wasibaguliwe” Akijibu moja ya maswali ya wananchi, Mhandisi wa Mazingira kutoka TANESCO Bw. Fikirini Mtandika alisema sheria na taratibu zote za mazingira zitazingatiwa wakati wote wa utekelezaji wa mradi chini ya usimamizi wa Baraza la Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira.

“TGDC inaandaa mikakati mbalimbali ya kupunguza na kuziondoa kabisa baadhi ya athari za mradi huu katika mazingira yetu” aliongezea Mhandisi Mtandika.

Wananchi wa maeneo yote yanayozunguka mradi wa jotoardhi wa Ngozi wameridhia hatua ya uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uzalishaji umeme na wako tayari kutoa ushirikiano. Kata zinazopitiwa na mradi huu ni Ijombe, Swaya-Mbeya vijijini, Swaya Rungwe na Ndanto.
Wananchi wakitoa maoni kwa wataalamu kutoka TGDC na TANESCO wakati wa mkutano wa kujadili athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kweye mazingira na kwa jamii.
Mtaalamu wa Sosholojia Bi. Vaileth Kimaro akizungumza na vikundi vya wanawake wakati wa kujibu maswali na kupokea maoni kuhusu athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kwa jamii na mazingira.
Mhandisi Leonard Masanja (aliyesimama kushoto) akijibu hoja za wananchi wa Kata ya Ndanto wakati wa mjadala wa athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kwa jamii na mazingira, aliyeshika kipaza sauti ni Afisa Maendelea ya Jamii wa Wilaya ya Rungwe Bi. Rachel Mbelwa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...