THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

WAZIRI MKUU AWAKARIBISHA WAIRAN KUWEKEZA NCHINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo  vya kuchakata mazao ya  kilimo na uvuvi.

“Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoa Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na uvuvi,” amesema.

Ametoa kauli leo (Ijumaa, Machi 17, 2017) alipokutana na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mheshimiwa Mousa Farhang kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake, hivyo wanahitaji  uwekezaji mkubwa kwenye sekta mbalimbali.

Pia Waziri Mkuu amewakaribisha raia wa Iran kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii ukiwemo mlima wa Kilimanjaro ambao unaongoza kwa urefu barani Afrika pamoja na mbuga nyingi zilizosheheni wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Farhang  ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi. Amesema Tanzania  ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani Afrika.

“Ufisadi na dawa za kulevya ni tatizo kubwa ambalo linazikabili nchi nyingi, hivyo kitendo cha Serikali ya Tanzania kupambana na tatizo hilo ni cha kupongezwa na kitaiwezesha kusonga mbele kiuchumi,” amesema.

Balozi Farhang amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na Iran ambao umedumu kwa miaka 40, hivyo ameiomba ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali.

“Tanzania na Iran wana uhusiano wa kihistoria ambao unadhihirishwa na uwepo wa Washirazi wengi husan visiwani Zanzibar ambao wanaasili ya Iran na maeneo ya kusini mwa Iran kuna Watanzania wengi hata muonekano wao ni wa Kitanzania,” amesema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekwenda nyumbani kwa marehemu Sir George Kahama Mikocheni jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa mjane Bi. Janneth Kahama pamoja na watoto na ndugu wa marehemu.

Baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu, Waziri Mkuu alitia saini kitabu cha maombolezo kabla ya kuzungumza na majane Bi. Janneth na baadae alijumuika na waombolezaji kwenye viwanja vya nyumba hiyo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Iran Nchini, Mhe. Mousa Farhang kwenye Makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam, Machi 17, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Iran Nchini, Mhe. Mousa Farhang kabla ya mazungumzo yao, kwenye Makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam, Machi 17, 2017.