WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuchakata mazao ya kilimo na uvuvi.

“Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoa Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na uvuvi,” amesema.

Ametoa kauli leo (Ijumaa, Machi 17, 2017) alipokutana na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mheshimiwa Mousa Farhang kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake, hivyo wanahitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta mbalimbali.

Pia Waziri Mkuu amewakaribisha raia wa Iran kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii ukiwemo mlima wa Kilimanjaro ambao unaongoza kwa urefu barani Afrika pamoja na mbuga nyingi zilizosheheni wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Farhang ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi. Amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani Afrika.

“Ufisadi na dawa za kulevya ni tatizo kubwa ambalo linazikabili nchi nyingi, hivyo kitendo cha Serikali ya Tanzania kupambana na tatizo hilo ni cha kupongezwa na kitaiwezesha kusonga mbele kiuchumi,” amesema.

Balozi Farhang amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na Iran ambao umedumu kwa miaka 40, hivyo ameiomba ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali.

“Tanzania na Iran wana uhusiano wa kihistoria ambao unadhihirishwa na uwepo wa Washirazi wengi husan visiwani Zanzibar ambao wanaasili ya Iran na maeneo ya kusini mwa Iran kuna Watanzania wengi hata muonekano wao ni wa Kitanzania,” amesema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekwenda nyumbani kwa marehemu Sir George Kahama Mikocheni jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa mjane Bi. Janneth Kahama pamoja na watoto na ndugu wa marehemu.

Baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu, Waziri Mkuu alitia saini kitabu cha maombolezo kabla ya kuzungumza na majane Bi. Janneth na baadae alijumuika na waombolezaji kwenye viwanja vya nyumba hiyo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MACHI 17, 2017.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Iran Nchini, Mhe. Mousa Farhang kabla ya mazungumzo yao, kwenye Makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam, Machi 17, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Iran Nchini, Mhe. Mousa Farhang kwenye Makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam, Machi 17, 2017

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...