Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Taraba amewataka wananchi wilayani humo kuchukua tahadhari na baa la ndege waharibifu wa mazao mashambani aina ya kwelea. Amesema tayari baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo yamevamiwa na ndege hao waharibifu wa mazao yakiwemo ya mtama, uwele, alizeti na mahindi yanayoanza kustawi.

Taraba ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alitoa tahadhari hiyo kwa wananchi mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya katika vijiji vya kata sita zilizopo wilayani humo. Akiwa amembatana na Ofisa Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji Wilaya, George Kessy na Ofisa Nyuki na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya (OCD), Emmanuel Gariyamoshi aliwatembelea wananchi wa kata za Uchunga, Mwadui Lohumbo, Idukilo, Ukenyenge, Mwamasele na Mwaweja.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kulinda mashamba yao na kuwafukuza ndege hao wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka ili kuwasaidia. Alisema tayari wilaya imeagiza ndege maalumu kwa ajili ya kumwaga sumu kwenye mazalia ya ndege hao ili wasiongezeke na kuleta madhara zaidi kwa mashamba ya wananchi.

“Serikali haijawatupa nawaomba wananchi tukae mashambani mwetu tulinde na kuwafukuza ndege hao wasile mazao yetu kwani tutapata hasara kubwa, hatujui hao kwelea kwelea watakuja lini, na hatujui hiyo ndege itakuja lini,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wananchi kuvuna haraka iwezekanavyo mazao ambayo tayari yamekomaa ili kutowapa mwanya ndege hao kufanya uharibifu wao na hivyo kuwapa hasara wakulima. Aliwataka wakulima wasihadaiwe na kuuza mazao yote kwa wafanyabiashara hali inayoweza kuwasababishia kukosa chakula baadaye na kulazimika kununua chakula kwa bei ya juu. Aliwaonya watu wanaofanya hivyo kwani huwaacha nyuma wakulima waliotoka jasho kulima mazao wakati wao wakineemeka kwa kuyauza mazao hayo kwa bei ya juu na kupata faida.

Kwa upande wake, Kessy alisema idara yake inawasisitizia wananchi wajenge utamaduni wa kuhifadhi chakula cha kutosha ghalani ili kiwasaidia katika siku zijazo na kuuza tu ile ziada inayobaki baada ya kutosheka. Aliwapa mbinu za kufukuza kwelea kwelea kwa kuweka vitambaa mithili ya bendera, sanamu za watu na kupiga madebe ili kuwafukuza ndege hao ili wapiti mbali ya mashamba wasiweze kufanya uharibu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba (katikati) akikagua mashamba katika vijiji vya Kata ya Mwadui Lohumbo. Wengine pichani kushoto ni Mkuu wa Polisi Kishapu, Emmanuel Gariyamosho na Afisa Nyuki, Revocatus Mboya.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akiwapungia mikono wakulima waliokuwa wakiendelea na shughuli shambani katika Kata ya Mwadui Lohumbo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...