Sehemu ya Makaburi ya Mashujaa wa Tanzania, waliokuwa mstari wa mbele kuitetea Tanzania, kuhakikisha wanamuondoa Nduli Idd Amini, hapa wakiwa wamelazwa 


MWISHO WA VITA VYA KAGERA.

Jumatano ya Aprili 11, 1979,

Rais wa Uganda Idi Amin Dada Oumee aliikimbia nchi yake na kwenda Libya na baadaye Saudi Arabia,  baada ya kushindwa vita dhidi ya Tanzania.

KISA CHA VITA

Uhusiano wa Tanzania na Uganda ulidorora tangu Januari 25, 1971, Idd Amin Dada(tamka Dadaa) alipoipundua serikali halali ya Rais Milton Obote aliyekuwa nchini Singapore kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola.

Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, akampa Obote na wenzake 2000 hifadhi ya kisiasa. Idd Amin hakufurahishwa na hilo kwani aliamini kwamba Nyerere anamuandaa Obote aje kumpindua, kwa hiyo akapanga kumdhibiti kabla hajampindua...akaivamia Tanzania.

MIKAKATI

Kanali, Abdu Kisuule, aliyekuwa mshirika wa karibu wa Idd Amin na kiongozi wa moja ya vikosi vya Uganda kwenye vita hiyo, aliongea na mtandao wa www.thecitizen.co.tz kwenye mfululizo wa makala za 'hadithi ambayo haikuwahi kusimuliwa ya vita vya Kagera' (The untold story of Kagera War by TZ Uganda top soldiers).

"Nilitumwa Ulaya kununua silaha, nilikuwa na wenzangu, Yekoko na meja Ndibowa. Tulikwenda Bilbao Hispania. Tulitumwa kununua vifaru, bomu aina ya Napalm ambalo ni maalumu kwa ajili ya kupambana na saba saba ya Tanzania(mtambo wa kurushia maroketi uliotengenezwa Urusi uliokuwa ukiitwa BM Katyusha rocket launcher), na ndege 112 za kuangushia mabomu.

Kwa bahati mbaya, kila tulipoenda, Tanzania ilitufuatilia na kuzima jaribio letu la kununua(Tanzania were tracking us and blocking our orders). Endapo tungefanikiwa kununua bomu la Napalm, habari ingekuwa habari nyingine kwa sababu Napalm ni bomu la moto ambalo huunguza kila kitu, linapotua. Wakati bado tukiwa Hispania, Tanzania ikavamia Uganda"
VITA YENYEWE

Januari 30, 1978, majeshi ya Idd Amin yalivamia Tanzania na kuvunja daraja la mto Kagera linalouunganisha mkoa wa Kagera na sehemu nyingine ya Tanzania. Amin akautangaza mkoa wa Kagera kama sehemu ya Uganda.

Rais wa Tanzania, Julius Nyerere akamsihi Amin kuondoa majeshi yake...Amin akakataa. Nyerere akaziomba jumuia za kimataifa kulaani uvamizi wa Idd Amin lakini dunia ikakaa kimya.

Nyerere akatangaza vita vilivyoanza Oktoba 30, 1978.

UWANJA WA MAPAMBANO

Nyerere alikusanya jeshi la wananchi lililoanza na askari pungufu ya 40,000 na kuongezeka mpaka 100,000 wakiwemo polisi, askari magereza, JKT na migambo

Jeshi hilo likaungana na vikundi mbalimbali vya waganda vilivyokuwa vikimpinga Amin ambavyo vilikutana mjini Moshi kwenye mkutano wao waliouita Moshi.

Mkutano huo ndiyo ulioanzisha jeshi lililoitwa Uganda National Liberation Army (UNLA).

Makundi haya ni pamoja na  Kikosi Maalum kilichokuwa chini ya Tito Okello( huyu ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar 1964) na David Oyite Ojok. Pia kulikuwa na kikundi cha FRONASA kilichokuwa chini ya Yoweri Museveni, pamoja kikundi kingine kama Save Uganda Movement.

Majeshi ya Tanzania yalikuwa na mzinga kutoka Urusi ulioitwa BM Katyusha rocket launcher (nchini ulikuwa ukifahamika kama saba saba) ambao ulivurumishwa moja kwa moja kwa majeshi Uganda. Majeshi ya Uganda yarudi nyuma.
MUAMMAR GADDAFI NA PALESTINA WAMSAIDIA IDD AMIN

Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, alituma wanajeshi 2,500 kumsaidia Idd Amin. Wanajeshi hao walikuwa na silaha za kisasa kama vifaru vya T-54 na T-55, BTR APC, BM-21 Grad MRL, artillery, MiG-21, pamoja na kombora la Tu-22.

Hata hivyo, walibya hao na wapalestina wakajikuta peke yao mstari wa mbele huku wanajeshi wa Uganda wakirudi nyuma. Askari wa Libya pamoja na Palestina wakatekwa

MWISHO WA VITA

Vita hiyo ilianza Oktoba 30, 1978 na kumalizika Aprili 11, 1979.
Baada ya vita hii, Gaddafi akamuomba Nyerere awaachie askari wake na yeye atampa pesa nyingi au mafuta. Nyerere akakataa akisema binadamu halinganishwi na chochote, akawaachia bure askari wale ambao walisifu sana jinsi walivyotendewa wakati walipokuwa mateka.
 Hayati Muammar Gaddafi akisalimina na wanajeshi wa jeshi la Idd Amin wakati wa vita ya Kagera. Idd Amin (katikati) akiwa anashuhudia.
 

Baadhi ya mabaki na kumbukumbu ya magari na mabomu yaliyotumika katika Vita ya Idd Amin mwaka 1978-79.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. kwa nini inaitwa vita ya kagera na iddi amin?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...