Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara imejipanga kujenga Kituo cha Ushonaji chenye lengo la kukuza sekta ya viwanda na kutoa ajira kwa vijana. 

Mpango huo umebainishwa hivi karibuni na Afisa Vijana wa Halmashauri hiyo, Mwakajila Emmanuel alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii juu ya maendeleo ya vijana waliopo katika Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan International. 

Mwakajila amesema kituo hicho kitachukua vijana mahiri katika ushonaji ambapo asilimia kubwa ya vijana ni wale waliopata mafunzo katika chuo cha VETA chini ya Mradi wa YEE kwani  wengi wao wanafanya  kazi nzuri lakini hawana vitendea kazi wala maeneo ya kufanyia kazi.

“Kituo hiki kitaajiri vijana wataalam wa ushonaji watakaokua wanashona sare za wanafunzi wa shule zote za Msingi na Sekondari za Wilaya yetu jambo ambalo litasaidia kulinda mzunguko wa fedha za ndani ya Halmashauri yetu badala ya kuzipeleka katika maeneo mengine,” alisema Mwakajila.

Afisa Vijana huyo ameongeza kuwa ili kuhakikisha jambo hilo linatimia, Halmashauri itatoa agizo kwa Wakuu wa Shule zote kuhakikisha wanaandika jambo hilo katika fomu za kujiunga na shule ili wazazi waweze kufahamu mahali ambapo sare hizo zinapatikana.

Amefafanua kuwa kazi ya Afisa Vijana ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili vijana katika shughuli zao za uzalishaji pamoja na upatikanaji wa huduma stahiki kwa ustawi wao zinatatuliwa.

Aidha, ametoa rai kwa vijana kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Halmashauri ili waweze kuimarisha biashara zinazowasaidia kupata fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao mbalimbali.

Pia ameyaomba mashirika binafsi kuendelea kujitolea kwa wingi kushirikiana na Serikali kusaidia vijana hasa wanaoishi katika mazingira magumu kwani misaada hiyo imekuwa ikiwawezesha vijana kupata mafunzo na ajira kwa ajili ya kuendeleza maisha yao na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Mradi huo wa miaka mitatu 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...