NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.

BAADHI ya wananchi kisiwani Pemba wameshauriwa kuacha siasa za visasi na chuki zinazochangia kuongezeka vitendo vya uhalifu wa mali na kuharibu heshima ya nchi kitaifa na kimataifa.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala katika mwendelezo wa ziara zake za kuimarisha uhai wa chama huko Tawi la CCM Kengeja, Mkoa kusini Pemba.

Alifafanua kwamba hali hiyo sio kwamba inaishia kuathiri uchumi na siasa za nchi peke yake bali vinaenda mbali kwa kuathiri maisha na undugu wa damu uliopo hata kabla ya kuanzishwa kwa mifumo ya kisiasa nchini.

Nasaha hizo alizitoa baada ya kuwepo kwa malalamiko ya uharibifu wa miundombinu ya maji safi na salama katika shehia hiyo, iliyoharibiwa na baadhi ya watu kwa kujenga zenge la kuzua maji yasiwafikie wananchi wa eneo hilo.
“ Serikali inarahisha huduma kwa wananchi kwa kuwajengea miundombinu rafiki ya upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na huduma nyingine muhimu lakini baadhi yenu wanaharibu kwa makusudi kutokana na masuala ya UCCM na UCUF, hilo sio sahihi kabisa lazima tubadilike kwa kuacha tabia hizo.”, alisema Dkt. Mabodi.

Hata hivyo alitoa wito kwa vyombo vya Dola kutoa taarifa na ripoti za kudhibiti vitendo hivyo kwa vyombo vya habari ili jamii ijue utekelezaji wake.

Aliwambia wanachama wa chama hicho kwamba waendelee kushikamana na kuwa watulivu na wasilipize visasi na badala yake waendelee kutenda wema na kuwaelimisha watu waohusika na hujuma hizo ili waweze kubadilika na kujiunga na chama hicho.

Aliwataka baadhi ya vijana wanashutumiwa kujihusisha na vitendo hivyo kuacha, na kutafakari kwa kina athari zake kwani zinawaumiza Watu wenye ulemavu, Wazee pamoja na wagonjwa waliopo hospitalini wanaohitaji huduma hizo wakati wote.

Pamoja na hayo alisisitiza umuhimu wa wanachama kushiriki katika zoezi la uchaguzi wa ndani ya chama na Jumuiya katika zoezi linaloendelea hivi sasa ili wapatikane viongozi wenye uwezo wa kukiletea chama ushindi wa ngazi zote za uchaguzi mwaka 2020.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu huyo alipongeza Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Mussa Ali Mussa kwa juhudi zake katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote licha ya kukabiliwa na vikwazo vya kisiasa kutoka kwa wapinzani.

Akitoa tathimini ya masuala ya ulinzi na usalama Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Salama Mbarouk Khatib alisema toka kumeanzishwa doria za mara kwa mara ndani ya eneo hilo vitendo vya uhujumu mali na miundombinu ya umma vimepungua.

Hata hivyo alisema na kutoa onyo kali kwa baadhi ya wananchi wanaoendelea na tabia ya kufunga Ng’ombe katika mifereji ya maji safi na kusababisha uharibifu, na kuongeza kuwa serikali itachukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuhusika na uhalifu huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanachama hao, waliwataka viongozi wa majimbo, jumuiya na chama kwa ujumla kufanya ziara za mara kwa mara katika mashina na Matawi ili kujua matatizo yanayowakabili wananchi pamoja na ufanisi na udhaifu wa utekelezaji wa shughuli za kisiasa katika ngazi hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...