Tanzania na Uganda zimefungua sura mpya ya ushirikiano baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo kusaini nyaraka inayoainisha maeneo mbalimbali ambayo nchi hizo zimekubali kushirikiana kwa pamoja ili kuinua uchumi wa mataifa yao.

Nyaraka hiyo iliyosainiwa leo jijini Arusha imetokana na Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda kilichofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 03 Aprili 2017. 

"Makubaliano haya yataongeza chachu ya uhusiano na ushirikiano wetu na Uganda, japokuwa tulichelewa kufanya kikao cha JPC tokea mkataba uliposainiwa mwaka 2007 nchini Uganda". Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga alisema alipokuwa akisoma hotuba ya kufunga.

Kikao cha JPC kilifanyika kwa kuzingatia makundi ya kisekta ambapo katika kila kundi, wajumbe waliainisha maeneo yenye maslahi kwa pande zote ambayo yanajumuisha pamoja na mambo mengine: uendelezaji wa miundombinu; kilimo; viwanda; biashara; uwekezaji; nishati; utalii; utunzaji wa mazingira; uvuvi; ufugaji; afya; elimu; utangazaji; madini na masuala ya kijamii.

Kikao hicho kilitarajiwa kuhitimishwa kwa kusainiwa mikataba sita lakini kutokana na mashauriano ya ndani ya baadhi ya mikataba kutokamilika, mikataba miwili ndio iliweza kusainiwa. Mikataba hiyo ni ushirikiano katika kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo na huduma za usafiri wa anga.

Mikataba minne iliyosalia ambayo inahusu ushirikiano katika usafiri wa reli, usafiri wa majini; utangazaji na ulinzi wa raia itasainiwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika hivi karibuni hapa nchini. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Nyaraka yenye maelezo ya masuala yote yaliyokubaliwa katika kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda. 
Waziri Mahiga na Mgeni wake, Mhe. Sam Kutesa wakionesha nakala za nyaraka za makubaliano mara baada ya kusaini. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Mkataba utakaotoa fursa kwa Tanzania na Uganda kushirikiana katika huduma za usafiri wa anga. 
Prof. Mbarawa na Mhe. Kutesa wakionesha nakala za mikataba mara baada ya kuisaini. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...