Na Daudi Manongi - MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesaini msaada wa shilingi Bilioni 490 usiokuwa na masharti yeyote kutoka Umoja wa Ulaya ikiwa ni msaada wa kibajeti kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka wa bajeti wa 2017/18.
Mkataba huo umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James kwa niaba ya Serikali na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Bw.Roeland van de Geer kwa niaba ya Umoja wa Ulaya.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini mkataba huo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James amesema Umoja wa Ulaya umetoa msaada huo kutokana na kuvutiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
“Nadhani mmeshuhudia utiaji saini huu ulioisha hivi punde na Umoja wa Ulaya wametuhakikishia kuendelea kutusaidia katika masuala ya misaada ya kibajeti pamoja na kuwa bega kwa bega na Serikali katika masuala mbalimbali ya maendeleo”, aliongeza Katibu Mkuu huyo.
Pamoja na hayo mpango wa pili wa maendeleo wa Taifa wa Bajeti ya mwaka 2017/18 pia utapewa msaada na umoja huo kwani wameuona mpango huo una tija na kuweka mkazo katika viwanda na kilimo.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Roeland Van de Geer amesema kuwa wameliangalia zaidi suala la utawala kama eneo kuu katika mpango wa ushirikiano na Tanzania na vilevile wanatazamia maendeleo zaidi katika maeneo ya kilimo,ujenzi wa barabara za vijijini na nishati.
“Mkataba ambao tumeusaini utaiwezesha Wizara ya Fedha na Mipango katika ukusanyaji wa mapato,zitaboresha uwajibikaji na utumiaji mzuri wa mali za Serikali, na Umoja wa Ulaya unasapoti azma ya viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano,”Aliongeza Roeland Van de Geer.
Amesema kuwa ushirikiano uliopo katika ya Tanzia na Umoja wa Ulaya ni mpana sana na utaendelea kuimarika zaidi katika kipindi hiki ambacho mageuzi ya sera yanahitajika.
 Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw.Dotto James akibadilishana mkataba wa kibajeti na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Bw.Roeland van de Geer mara baada ya kusaini mkataba huo Jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Bw.Roeland van de Geer akizungumza jambo na waandishi wa habari juu ya msaada wa shilingi bilioni 486.9 uliotolewa na umoja huo kwa Serikali ya Tanzania ili kusaidia Bajeti.Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw.Dotto James.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw.Dotto James akitoa ufafanuzi kwa wahandishi wa habari juu ya msaada wa shilingi bilioni 486.9 ambao Serikali imeupata kutoka umoja wa ulaya (EU) kwa ajili ya kusaidia Bajeti.Kushoto kwake ni Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Bw.Roeland van de Geer.Picha na Daudi Manongi-MAELEZO.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Kwa nini tunapokea misaada tu kila siku? Hao wanaotupatia misaada wanafaidika nini na wanataka nini kutoka kwetu? Tumekua tukipatiwa misaada miaka mingi na hali yetu inazidi kuwa mbaya. Sio kila misaada ina nia nzuri. Tujiamini sisi wenyewe kwani tunaweza kujiendesha wenyewe kwa rasilimali zetu ambazo kwa sasa hao wanaotupatia misaada wanazichukua huku sisi tukisubiri kupatiwa misaada.

    ReplyDelete
  2. Ndugu mja mjoli, hayo unayosema, na tahadhari hizo, yalifafanuliwa vizuri katika "Azimio la Arusha." Lakini zile zilikuwa enzi za chama makini cha TANU, kilichokuwa na mwelekeo wa mapinduzi. Leo, baada ya CCM kutupilia mbali mwelekeo ule wa mapinduzi, kilichobaki ni viinimacho.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...