MFUKO wa uwekezaji wa pamoja wa UMANDE UNIT TRUST (UUT) leo umezindua rasmi mpango-mkakati wake wa kifedha utakaowawezesha wawekezaji wadogo na wale wenye kipato cha chini na cha kati waweze kununua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kupitia njia ya vipande.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CORE Capital Limited ambayo ndio iliyobuni mfuko huo, Bw George Fumbuka  alisema kiwango cha chini cha ununuzi wa hisa za Vodacom ni 85,000/= (hisa 100 kwa 850/= kila hisa), kwa mkupuo kinaweza kuwa kiasi kikubwa kwa wawekezaji wadogo wadogo, wa kipato cha chini.

“Mantiki ya mkakati huu ni kuwakusanya pamoja wale wote wenye mitaji midogo ili waweze kwa pamoja kufikia viwango vinavyohitajika katika ununuzi wa hisa za VODACOM. Kima cha chini ni shilingi 13,500 tu, yaani vipande 100 vya shilingi 135/= kila kimoja. Dhana hii si mpya kwa Watanzania; mara nyingi tu hutumika kwenye shughuli za pamoja, huitwa “UMOJA NI NGUVU”.’’ Alisema

Alisema mpango huo pia utatoa fursa kwa wawekezaji wa kigeni wakiwemo watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) kuweza kunufaika na hatua hiyo ya serikali kwa kuwa uuzwaji wa hisa hizo kupitia soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) hautoi fursa kwa wawekezaji wa kigeni.

“Kwa kuwa mauzo ya hisa hizo hapa nchini hayahusishi wawekezaji wa kigeni wakiwemo watanzania wanaoishi nje yaani Diaspora, milango ipo wazi kwao kupitia mfuko wa uwekezaji mtaji wa Umande (Umande’s capitalisation fund),utakaowawesha kununua vipande badala ya wao kwenda moja kwa moja kwenye soko la hisa,’’ alisema.

Zaidi Bw Fumbuka aliwahakikishia walengwa wa mpango huo kuhusiana na uhakika wa wao kujipatia gawio na faida zitokanazo na mtaji (dividends and capital gains) kama kawaida kwa kuwa thamani ya vipande itakwenda sambamba na thamani ya hisa za kampuni hiyo ya huduma za simu za mkononi.

“Mpango mkakati huu una baraka zote za Kampuni ya Vodacom na za Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) chini ya Kanuni za Mifuko ya Uwekezaji ya mwaka 1997.” Alibainisha.

Hata hivyo alifafanua kwamba watakaopitia mkakati huo, wawe ni wawekezaji wadogo wadogo au wale wa nje, hawataweza kumiliki hisa za VODACOM moja kwa moja; badala yake watamiliki vipande vya Mfuko utakaopatikana kwa michango yao.

“Kwa maana hiyo Mfuko wa UUT ndiyo utanunua hisa za VODACOM kwa niaba yao na watafaidi matunda ya uwekezaji kwa njia hiyo. ‘’ alisema huku akiongeza kuwa Vipande vitanunuliwa kwa njia ya simu tu: *150*36#, huku kima cha chini kikiwa ni Tsh 13,500/=.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CORE Capital Limited ambayo ndio iliyobuni mfuko huo, Bw George Fumbuka (katikati) akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo mpango-mkakati unaoendeshwa na kampuni hiyo kupitia Mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa UMANDE UNIT TRUST (UUT) utakaowawezesha wawekezaji wadogo na wale wenye kipato cha chini na cha kati waweze kununua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kupitia njia ya vipande. Wengine ni Meneja wa Mfuko huo Bi Sandra Felician na Naibu wake Bi Nkunde Shoo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...