Na Lulu Mussa, Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, hii leo amekutana na
taasisi zizohusika na uratibu na usimamizi wa kemikali hapa nchini.
Akiongea na Taasisi hizo, Waziri Mpina amewaagiza watendaji hao kudhibiti na
kusimamia kemikali hatarishi nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu usafirishaji, usambazaji
na matumizi ya kemikali hizo hapa nchini kwa namna bora zaidi.
Waziri Mpina amezitaka taasisi hizo kutoa taarifa za utendaji wa kazi kila robo ya
mwaka kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimizi wa Mazingira kwa mujibu wa Sheria
ya Mazingira kifungu namba 170. “Nawaagiza kuwasilisha takwimu za kemikali
zinazozalishwa nchini, zinazoagizwa au kusafirishwa nje ya nchi, pamoja na kuainisha
viwanda vinavyozalisha kemikali vilivyosajiliwa na maghala yaliyosajiliwa kuhifadhi
kemikali hizo” alisisitiza Mpina.
Katika kikao hicho Waziri Mpina pia ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira nchini ndani ya miezi miwili kuandaa muongozo na kuupitisha katika
hatua zote wa namna bora ya kuteketeza taka hatarishi bila kuathiri mazingira.
Aidha Waziri Mpina ameagiza kuandaliwa kwa andiko litakalobainisha umuhimu wa
kuteketeza taka hatarishi. “Kama taifa ni lazima tuwe na “dedicated Incinerator” kubwa
kutekeza taka hizo hatarishi kwa kuzingatia taka zinazozalishwa hapa nchini” Mpina
alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini,
Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania, Tume ya Nguvu za Atomiki, Taasisi ya
Utafiti ya Viuatilifu katika Kanda za Kitropiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa, OSHA na
Mkemia Mkuu wa Serikali kwa pamoja wametakiwa kuanda Hati ya Makubaliano ya
kuratibu utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuhuisha Sheria zao na
kuleta mapendekezo Serikali ya vifungu vya kufanyiwa marekebisho.
Taasisi alizokutana nazo ni pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira nchini (NEMC), Taasisi ya Nguvu za Atomiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa
na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Bw. Justine Ngaile Mkurugenzi wa Kinga na Mionzi kutoka Tume ya Atomiki
akiwasilisha mada kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Luhaga Mpina.
Waziri Mpini alikutana na Taasisi zinazohusika na usimamizi wa kemikali kujadilili
mkakati wa pamoja wa kusimamia kemikali nchini.
Baadhi ya wataalamu kutoka Taasisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya
Chakula na Dawa na Tume ya Nguvu za Atomiki wakifuatilia majadiliano na Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina (hayupo
pichani), kikao kazi hicho kimefanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...