Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amewataka
wananchi wamuunge mkono Rais John Mafuguli, katika kuhakikisha
anasimamia rasilimali za watanzania na kufanikisha maendeleo ya sekta
mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mofuga, wakati inakaribia miaka miwili ya utawala wa
Rais Magufuli amefanikisha maendeleo mengi ambayo yangeweza kufanyika
kwa kipindi cha utawala wamuda wa miaka 40.
Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Mbulu, alisema miongoni mwa
maendeleo hayo ni kuzindua na kuanza kwa ujenzi wa reli ya umeme,
kuhamisha makao makuu ya nchi Dodoma mpango uliodumu tangu mwaka 1973
na kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara za ghorofa kwenye jiji la
Dar es salaam.
Alisema amefanikisha kuongezeka kwa pato la Taifa kupitia ukusanyaji
wa kodi kutoka sh850 bilioni kwa mwezi alipokuwa anaingia madarakani
hadi kufikia sh1.2 trilioni kwa mwezi hivi sasa.
Alisema pia Rais Magufuli amefanikisha ununuzi wa ndege na kufufua
shirika la ndege la ATCL, kutoa elimu bure kwa shule za msingi na
sekondari jambo linaloongeza usajili wa wanafunzi mara mbili.
"Amegundua watumishi wenye vyeti feki 9,932 na watumishi hewa 19,706
ambao mishahara yao ilikuwa inatumiwa na watu wachache badala ya
kupelekwa kwenye shughuli za maendeleo za wananchi ikiwemo elimu, afya
na maji," alisema Mofuga.
Alisema Taifa lilishuhudia historia nyingine baada kupokea ripoti ya
tume aliyounda ya kuchunguza mchanga wenye dhahabu (makinikia) yenye
wajumbe nane wenye taaluma mbalimbali za uhandisi na kuchukua hatua
stahiki mara baada ya kupokea.
"Kwenye taarifa hiyo ilibainika kuwa thamani ya madini yote kwenye
makinikia ni makontena 277 yenye thamani ya sh829.4 bilioni kwa
viwango vya wastani na viwango vya juu ni sh1.4 bilioni yaani dhahabu
iliyokuwa kwenye makontena 277 ni sawa na lori mbili za tani saba ba
pick up tani 1.5," alisema Mofuga.
Alisema Taifa lilikuwa linahitaji kiongozi aina ya Rais Magufuli kwa
muda mrefu na kutokana na utekelezaji huo unaofanyika wananchi
wanatakiwa kumuunga mkono ili aongeze jitihada za kuhakikisha Tanzania
inafika kwenye nchi ya maziwa na asali.
Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo Yohana Amnaay alisema pamoja na
jitihada hizo za Rais Magufuli pia mkuu huyo wa wilaya ya Mbulu
Mofuga, amekuwa na utaratibu mzuri wa kutatua kero za jamii hasa
migogoro ya ardhi kwa kukutana na wananchi.
"Kila alhamisi DC wetu amekuwa na utaratibu wa kukutana na wananchi
hivyo kupitia nafasi hiyo jamii imekuwa inatatuliwa kero zake kuliko
kukaa na kusubiri viongozi wakubwa wafike Mbulu ndiyo wananchi
wafikishe malalamiko yao kwao," alisema Amnaay.'
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...