Na Beatrice Lyimo na Fatma Salum-MAELEZO
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaongoza maelfu ya Watanzania kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa Shule ya Msingi Lucky Vicent waliofariki kwa ajali ya gari Mei 6 mwaka huu Mkoani Arusha.
Katika tukio hilo lililofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Makamu wa Rais ametoa salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa Mkuu wa Mkoa, Wazazi na wote walioguswa na msiba huu.
“Shukrani kwa Rais wa Kenya na Wakenya wote kwa ujumla kwa kujumuika na Watanzania katika kuomboleza msiba huu ulioukumba taifa, ambapo Rais Uhuru Kenyata amemtuma Waziri wa Elimu wa nchi hiyo kuwakilisha Wakenya katika kuomboleza msiba huu” anasema Makamu wa Rais.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Elimu, Jeshi la Polisi na wazazi kulinda Sheria za Usalama barabarani ili kulinda maisha na ndoto za watoto. “Msiba huu umegusa kila Mtanzania, hivyo tuzidi kuwaombea Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, hivyo tujipe moyo na nguvu kwamba hili limetokea na kwa Mwenyezi Mungu tujirudishe” ameongeza Makamu wa Rais.
Hata hivyo Makamu wa Rais ametoa wito kwa madereva wa magari mbalimbali kuwa makini na waangalifu katika vyombo vya moto wanavyovitumia.
Aidha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako ametoa pole kwa wazazi wote waliondokewa na watoto na ndugu zao, wafiwa na watanzania wote walioguswa na msiba huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amewapa pole wazazi na wanajumuia wote na kusema kuwa kama kuna kitu kinatuunganisha sote ni kifo kwani kila binadamu ana mwisho wake.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe amesema kuwa Mwenyezi Mungu ametoa nafasi ya kutafakari umoja wetu na ushirikiano wetu kama taifa kupitia msiba huo.

Vilevile Waziri wa Elimu kutoka nchini Kenya Dkt. Fred Matiang’I amesema kuwa Kenya itaendelea kuwa pamoja na Watanzania kwenye kipindi hiki kizito cha msiba huo mzito ulioukumba taifa.
Mbali na hayo Rais Dkt. John Magufuli kwenye ukurasa wake wa Twitter amesema kuwa amepatwa na uchungu na majonzi makubwa alipoyaona majeneza ya watoto na walezi wao waliopoteza maisha katika ajali ya basi huko Arusha.
“Tumepoteza mashujaa wetu katika elimu, tuwaombee na tuendelee kuwa na subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Rais Magufuli.
Wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent walipata ajali ya basi Mei 6, mwaka huu Mkoani Arusha walipokuwa wakienda kufanya mtihani wa ujirani mwema.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa zoezi la kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Visent katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akitoa pole kwa ndugu na jamaa wa marehemu waliofika katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha kwa ajili ya kuaga miili hiyo.
Miili ya wanafunzi 32, walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Visent ikiwa katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha kwa ajili ya kuombewa pamoja na kuagwa leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akitoa heshima za mwisho kwenye miili ya wanafunzi 32, walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Visent katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akiwafariji ndugu na jamaa wa marehemu waliofika kuaga miili ya ndugu zao leo katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Kiserikali na chama wakiwa kwenye 
uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha wakati wa kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Visent.

Wanafunzi wa shule ya Lucky Visent wakiwa kwenye majonzi wakati wa kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Visent katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.

Baadhi ya wakazi wa jiji la Arusha wakiwa 
 katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha kwa ajili ya kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Visent waliofariki kwenye ajali. HABARI ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Ni masikitiko makubwa kuwapoteza vijana hawa. Ila ni masikitiko makubwa zaidi kwamba kwa mara nyingine tena barabara na magari yetu yanatuangamiza bila ya sisi wenyewe kutanabahi na kuchukua hatua madhubuti.
    Twamwomba Allah awapokee vyema watoto hawa.Ameen.
    Lakini nasi tuliobaki iwe sasa ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti. Huku katika nchi zilizoendelea wenzetu wameweza kupunguza madhara ya ajali kwa asilimia kubwa sana. Kwanini sisi tusisome kutoka kwao. Yumkini watoto hawa hawakuwa wamepewa elimu ya kutosha kabla ya kuingia chomboni. Yawezekana sana, bali ndivyo hasa ilivyo, safari haikutanguliwa na risk assessment wala vijana hawakufunga mikanda ndani ya basi. Naamini mikanda ingepunguza vifo japo kwa asilimia 30.
    Viongozi wetu mpaka lini mtaona haja ya kujifunza. Kwanini watz wamekuwa wakisubiri kifo tu. Hivi ni kweli kuwa hakuna kiongozi wa wizara ya elimu au jeshi la trafiki anaeelewa masuala ya child protection?
    Karne hii?
    Tafadhali viongozi wakuu tafuteni suluhisho la mabalaa haya. Suluhisho lipo na siamini kuwa watz ni watu wa kufa kufa ovyo tu kama sisimizi.
    Mndengereko ukerewe

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...