Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini

1. UTANGULIZI

(i) Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Gedleyihlekisa Zuma anatarajiwa kufanya Ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini, kuanzia tarehe 10 hadi12 Mei 2017, kwa mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(ii) Ziara hii inafanyika baada ya Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Zuma kukutana mjini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

(iii) Mheshimiwa Rais Zuma anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 10 Mei 2017, jioni na kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli. 

(iv) Ziara hii itatoa fursa kwa Viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara. Ujio wa Mheshimiwa Rais Zuma ni fursa nzuri sana ya kuendelea kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano mazuri naya kihistoria kati ya nchi zetu mbili. 

(v) Mheshimiwa Rais Zuma anafuatana pia na wafanyabiashara takribani 80. Hii ni fursa muhimu sana katika kukuza mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Hivyo, tarehe 11 Mei 2017, kutakuwepo na Kongamano la Wafanyabiashara katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (JINCC).

(vi) Ziara ya Mheshimiwa Rais Zuma inaenda sambamba na vikao vya Tume ya Pamoja ya Marais (Bi-National Commission - BNC) kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Mkutano wa Marais umepangwa kufanyika tarehe 11 Mei, 2017. Mkutano huo utatanguliwa na Kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 10 Mei, 2017 na kikao cha Makatibu Wakuu kitafanyika tarehe 8 na 9 Mei, 2017.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu Ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini Mhe. Jacob Zuma, ambaye atawasili nchini kwa ziara ya siku 3. Pamoja na mambo mengine, Rais Zuma pia atatembelea Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha tiba ya ugonjwa wa moyo (Jakaya Kikwete Cardiac Institute), na pia kufungua rasmi Ubalozi wao hapa nchini. 
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Suleiman Salehe, akimsikiliza Waziri Mahiga (Hayupo pichani) katika mkutano na waandishi wa Habari 
Sehemu ya waandishi wa habari wakinukuu maeneo mbalimbali yaliyotajwa na Waziri Mahiga kwenye mkutano na waandishi wa habari. 
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...