Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema iwapo Mpango wa Huduma ya Afya ngazi ya Jamii utatumika vizuri utasaidia kuokoa Afya na maisha ya wananchi wengi Mkoani humo.

Mtaka ameyasema hayo katika kikao kilicho wahusisha Viongozi ngazi ya Mkoa,Wilaya, watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi, Itilima na Mji wa Bariadi, ambacho kililenga kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa mpango wa huduma ya Afya ngazi ya Jamii mkoani humo.

Mtaka amesema mwamko wa kupata huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa wananchi katika maeneo mengi mkoani humo uko chini, hivyo mpango huu wa kutoa huduma ngazi ya kaya utasaidia kuhamasisha wananchi kutafuta huduma za afya katika vituo hivyo badala ya kutegemea tiba za kienyeji.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.

“Tukitumia huduma hii ya Afya Majumbani vizuri itasaidia sana, tukifika mahali ambapo jamii yetu itapata mwamko wa kupata matibabu katika vituo stahiki vya afya tutakua tumeokoa jamii yetu, kwa sababu bado wapo wanaoamini kupata matibabu katika tiba za kienyeji; tungehitaji wananchi wetu huduma ya kwanza kwenye afya iwe vituo vyetu kutolea huduma za afya na siyo tiba mbadala” amesema Mtaka.

“........kwa sisi ambao tunatengeneza Mkoa wetu katika Uchumi, Uchumi ni Afya wananchi hawawezi kufanya kazi wakajenga uchumi kama hawatakuwa na afya njema” alisisitiza. Aidha, Mtaka amewataka Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji kufanya utambulisho wa kutosha wa wahudumu wa afya ya Msingi ngazi ya jamii watakaokuwa wakitoa huduma kwa wananchi katika maeneo yao ili wataalam hao wasije wakapata madhara yoyote wakati wakitekeleza majukumu yao.
Dkt.Ama Kasangala kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akizungumza na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani Simiyu.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amewataka wananchi kuachana na taratibu za kimila zinazoathiri utendaji wa watumishi wa Umma ikiwemo kutumia mahakama za kimila (dagashida) na akawataka viongozi hao kuwasaidia wananchi kubadilika ili wahudumu wa afya ngazi ya Jamii watakaopelekwa katika maeneo yote ya mkoa huo watekeleze majukumu yao bila vikwazo vyovyote.

Wakati huo huo Mtaka ameomba Shirika lisilo la Kiserikali la AMREF lisaidie katika kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii walipewa mafunzo, ili wasaidie kutoa huduma na kupunguza changamoto ya upungufu wa watoa huduma wakati Serikali ikiendelea kushughulikia suala hilo.
Baadhi ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.

Vile vile ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa afya ikiwemo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kushughulikia suala la upatikanaji wa vifaa ili watoa huduma ngazi ya jamii watakapowafikia wananchi waweze kutoa huduma stahiki kwa wakati.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...