Na Nuru Juma-MAELEZO
Serikali
inamkakati wa kuhakikisha inajenga Magereza katika maeneo yenye
uzalishaji mkubwa wa kilimo ambayo pia yana ukubwa wa kutosha ili kazi
ya kuwarekebisha wafungwa iwe rahisi kufanyika huku shughuli za
uzalishaji zikiwa zinaendelea.
Hayo
yamesemwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi
Mhe. Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mhe Devotha Minja Mbunge
wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro.
“Magereza
hayo yatajengwa katika maeneo yenye Kilimo na yatakuwa ni kwa ajili ya
watu waliokwisha hukumiwa huku yale Magereza ya mijini yawe kwa ajili ya
mahabusu tu ili wawe karibu na Mahakama,”alisema Mwigulu.
Aliongeza
kuwa mkakati huo wa Serikali ni wa muda mrefu na wanahitaji kufanya
hivyo ili kurahisisha shughuli za maendeleo zinazofanywa na wafungwa na
pia kupunguza msongamano wa wafungwa katika Magereza.
Hili
pia linatokana na tamko la Mh.Rais Dkt John Pombe Magufuli alilowahi
kulitoa hivi karibuni kuwa wafungwa wako katika kutumikia adhabu hivyo
wanatakiwa kufanya kazi hasa za kilimo ili kwanza kujipatia chakula na
sio kukaa tu bure na kusubiri kila kitu wafanyiwe na serikali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...