​Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepiga marufuku utaratibu wa kufutarishana na kupeana chakula kilichotayarishwa nyumba moja kwenda nyengine katika mwezi huu wa Ramadhani baada ya kubainika kuwepo kwa mripuko wa maradhi ya Kipindupindu katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Wizara ya Afya Mnazimmoja, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo Riziki Pembe Juma alisema lengo la Serikali kuweka marufuku hiyo ni kujaribu kudhibiti maradhi hayo yasisambae zaidi.

Alizitaja hatua nyengine ambazo Serikali imechukua ni kuzuia uuzwaji holela wa vyakula vya kupika na vya majimaji katika maeneo yasiyorasmi na kuwashauri wananchi kuchemsha maji ya kunywa ama kuyatia dawa ya klorini, kukosha vizuri matunda na mboga za majani kwa maji yaliyochemshwa.

Alisema uchunguzi uliofanywa kwa wagonjwa waliolazwa kwa sababu  ya  kuharisha na kutapika katika vituo vya afya na hospitali mbali mbali umebainisha kuwepo ugonjwa wa kipindupindu aina ya Ogawa 01.

Waziri Riziki ameweka wazi kupokewa wagonjwa 23 waliopatikana na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu na tayari Wizara ya afya imefungua kambi maalum ya matibabu katika eneo la Chumbuni.

Aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi na ugonjwa huo ni Wilaya za Mjini na Magharibi hasa katika Shehia ya Kinuni, Darajabovu, Mtoni Kidatu, Chumbuni, Mwanakwerekwe, Fuoni na Kwarara.

Hata hivyo Kaimu Waziri wa Afya amethibitisha kuwa hadi sasa hajapatikana mgonjwa kutoka kwenye maeneo ya ukanda wa pwani na zile kanda za utalii au kwenye hoteli za kitalii na Kisiwa cha Pemba.

Amewaomba wananchi kuimarisha usafi katika maeneo wanayoishi na watakaona dalili za ugonjwa huo wakimbilie vituo vya afya huku Serikali imejipanga kwa dawa na wafanyakazi na kutoa elimu ya afya katika kukabiliana na maradhi hayo .

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Abdalla amewasisitiza wafanyabiashara wadogo wadogo kufuata taratibu zilizowekwa na Wizara ikiwemo kupima afya kabla ya kuanza biashara na kuandaa mazingira mazuri ya sehemu watakazofanyia biashara zao.
Kaimu Waziri wa Afya Riziki Pembe Juma akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mripuko wa maradhi ya kipindupindu Zanzibar huko Makao Makuu ya Wizara ya afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohd Abdalla akijibu masuala  yaliyoulizwa na waandishi wa habari katika mkutano huo.
Picha na Makame Mshenga.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya Serikali na binafsi wakimsikiliza Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar katika mkutano uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...