Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

MCHUNGAJI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, George Milulu ameieleza Mahakama ya  kuwa alisikia uvumi kwamba Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Josephat Gwajima amefariki dunia.

Mchungaji Milulu amedai hivyo leo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa utetezi wake dhidi ya shtaka linalomkabili yeye na wenzake la kukutwa na silaha.

Akiongozwa na Wakili wake Peter Kibatala, amedai kuwa, alipata taarifa ya uvumi kwamba Askofu Josephat Gwajima amefariki katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.

Akielezea ilivyokuwa amedai yeye ni Mchungaji wa Kanisa la ufufuo na uzima tangu mwaka 2008.

Amedai kuwa, Machi 29, 2015 alikuwa hospitali ya TMJ ambapo alikuta watu ni wengi, lakini muda mfupi baadaye waliamuliwa na Polisi wakae eneo moja wakiwemo waliokuwa waumini waliokuwa juu ya ghorofa washuke chini.

Shahidi huyo ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo ameongeza kuwa kabla hawajajua sababu ya kukusanyika upande mmoja walipewa amri nyingine ya kuingia ndani ya gari la Polisi aina ya Land cruiser na kupelekwa kituo cha Oysterbay.

 Wakili Kibatala alimuuliza kama alipokuwa TMJ aliwahi kuliona begi lenye silaha ambalo lilitolewa mahakamani kama kielelezo, alijibu kuwa hakuwahi kuliona.

Naye shahidi George Mzava alieleza kuwa hajawahi kukutwa na begi lolote katika hospitali ya TMJ kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka. Alidai kuwa baada ya kukamatwa na Polisi walifikishwa Oysterbay ambapo waliamriwa wavue mikanda na kuanza kuhojiwa mmoja mmoja.

Aidha shahidi huyo ameieleza mahakama yeye na wenzake hawakuiona hiyo silaha wanayodaiwa kukutwa nayo wala begi la Askofu Gwajima. Amedai kuwa kwa mara ya kwanza kuiona silaha hiyo ni pale ilipopelekwa mahakamani hapo kama kielelezo pamoja na risasi zake.

Hata hivyo, wakili wa serikali Shadrack Kumar alipomuuliza shahidi huyo kuwa yeye ni mlinzi wa Askofu Gwajima ama ni Askofu, alijibu kuwa ni Askofu.

Kesi hiyo itaendelea kesho.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni  Askofu Gwajima, George Mzava, Yekonia Bihagaze (39) na  Georgey Milulu ambao wote wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa wakimiliki Bastola aina ya Berretta pamoja na risasi 20 kinyume cha sheria.

Wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A walikutwa wakimiliki Bastola aina ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...