Na Benny Mwaipaja, WFM

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Tao Zhang (kushoto) ameahidi kufungua madirisha ya mikopo kwa nchi ya Tanzania kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali za kukuza uchumi.

Bw. Zhang aliyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), katika ofisi za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.

“Shirika la Fedha la Kimataifa limeziona jitihada za kukuza uchumi wa nchi ambapo mpaka sasa Tanzania inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki na ipo juu ya wastani wa ukuaji wa uchumi Barani Afrika” Alisema Bw. Zhang.

Ameishauri Serikali kuendelea kushirikiana na Sekta binafsi  katika ukuaji wa Uchumi ili uchumi huo uwe endelevu. Aidha ameitaka Serikali kuwa na mfumo shirikishi wa kifedha utakao wanufaisha wananchi wengi.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), amesema kuwa juhudi za Tanzania  kwa sasa ni  kuchochea ukuaji wa Kilimo na kuongeza uzalishaji wenye tija

“Umasikini haujatatuliwa kwa kiwango ambacho Serikali ingependa kukiona, kwa kuwa mpaka sasa watu walio katika  umasikini na ukosefu wa huduma za lazima ni takribani asilimia 34.4 “, aliongeza Dkt. Mpango

Kama nchi imeamua kwenda kwenye uchumi wa kati na jambo ambalo linatiliwa mkazo ni upatikanaji wa umeme wa kutosha na wenye bei nafuu .

Amesema kuwa Serikali imefanya juhudi za kupeleka umeme mpaka vijijini lakini bado kazi hiyo haijakamilika. Pia suala la miundombinu ya ya usafirishaji ni changamoto, ukiwemo usafiri wa reli kutoka Mashariki hadi Magharibi mwa nchi ambao ni wazamani na umeharibika.

“Serikali imeamua kujenga Reli yenye kiwango cha Kimataifa (Standard gauge)  ambayo ni ya gharama, na kwa makadirio ya awali zinahitajika Dola Bilioni 7.6, lakini umechukuliwa uamuzi huo ili kuharakisha Maendeleo”aliongeza Dkt. Mpango 

“Tayari tumeanza ujenzi wa reli hiyo kwa fedha za ndani kwa takribani Kilometa 200 kutoka Dar es salaam mpaka Morogoro na tutaendelea na ujenzi kadri fedha zinavyo patikana” alifafanua Waziri Mpango .

Amesema kuwa, kumekuwa na tatizo la ahadi za Wahisani kutotekelezwa kwa wakati jambo linalofanya baadhi ya shughuli za maendeleo kutotekelezwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) anaeziwakilisha nchi 23 za Afrika, Bw. Maxwell Mkwezalamba, alisema ni  vema Serikali ikaendelea kuangalia vipaumbele  katika ujenzi wa miundombinu ili iweze kuchochea uchumi.
“Suala la ajira hasa kwa vijana linatakiwa kufanyiwa kazi na pia kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa Sekta Binafsi kwa kuwa Sekta Binafsi imekuwa na mchango mkubwa katika Maendeleo kwa nchi nyingi Duniani” Alishauri Bw. Mkwezalamba.
Ameishauri Tanzania kuendelea kuwekeza kikamilifu katika Sekta ya Elimu kwa kuwa ni moja ya eneo ambalo kama likifanyiwa kazi kikamilifu litaleta Matokeo chanya na ya haraka katika ukuaji wa Uchumi.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo, Waziri Mpango, amesema Serikali imeendelea kuhakikisha kunakuwa na viwanda vingi ili vijana wengi waweze kupata ajira. Aidha tayari Tanzania imeanza kutekeleza Elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kupata elimu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...