Jitihada za Wizara ya Nishati na Madini za kuhakikisha umeme unafika na kusambaa maeneo ya vijijini zimetambuliwa kimataifa hali iliyopelekea Serikali kupokea Tuzo ya Uwezeshaji wa Mazingira Bora ya Upatikanaji wa Umeme Vijijini kwa Nchi zinazoendelea.

Serikali imetunukiwa Tuzo hiyo mwezi Machi, 22 na Taasisi ya Kimataifa ya Alliance for Rural Electrification yenye Makao Makuu yake nchini Ubelgiji ambayo ilipokelewa na Meneja Miradi wa Kampuni ya Umeme ya Ensol, Prosper Magali kwa niaba ya Serikali katika hafla ya utoaji tuzo iliyofanyika Lisbon, Ureno. Magali pia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Nishati Jadidifu (TAREA).
Meneja Miradi wa Kampuni ya Umeme ya Ensol, Prosper Magali (kushoto) akipokea Tuzo ya Uwezeshaji wa Mazingira Bora ya Upatikanaji wa Umeme Vijijini kwa Nchi zinazoendelea kwa niaba ya Serikali kutoka kwa Mwenyekiti wa Sera ya Mtandao wa Kimataifa wa Nishati Mbadala (REN21) yenye makao makuu yake nchini Ufaransa, Profesa Arthouros Zervos.

Akikabidhi Tuzo hiyo Jijini Dar es Salaam, kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo; Magali alisema Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wa Serikali ya Tanzania wa kufikisha huduma ya umeme maeneo ya vijijini pamoja na uwezeshaji wa mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji wanaosambaza umeme katika maeneo ya vijijini.

“Kwa mwaka huu, Serikali yetu imetambuliwa kwa kufikisha umeme vijijini na juhudi zake za kuhakikisha kunakuwa na mzingira rafiki kwa watoaji na wasambazaji wa huduma ya umeme vijijini,” alisema Magali.
Meneja Miradi wa Kampuni ya Umeme ya Ensol, Prosper Magali pamoja na washiriki kutoka nchi mbalimbali wakionesha Tuzo walizopokea kutoka kwenye Taasisi ya Kimataifa ya Alliance for Rural Electrification katika hafla ya utoaji tuzo iliyofanyika Lisbon, Ureno.

Kwa upande wake Dkt.Mhandisi Pallangyo aliipongeza kampuni ya Ensol kwa kupokea tuzo kwa niaba ya Serikali na kuahidi kuendeleza ushirikiano na kampuni zote zinazojihusisha na usambazaji wa umeme maeneo ya vijijini.

Alisema Serikali itaendelea kuandaa mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kutimiza azma ya kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma ya Nishati ya Umeme.
Aidha, Dkt. Mhandisi Pallangyo alizitaka kampuni nyingine zinazoshughulika na uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini kujiunga na Taasisi za Kimataifa ikiwemo ya Alliance for Rural Electrification ili kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye Taasisi hizo.

Makabidhiano hayo yalishuhudiwa na watendaji wa Wizara na Taasisi zake wakiongozwa na Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Ensol, Hamis Mikate.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akipokea Tuzo kutoka kwa Meneja Miradi wa Kampuni ya Umeme ya Ensol, Prosper Magali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...