Ubalozi wa Marekani imeingia rasmi katika ubia
na Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar kwa kusaini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kuwa na programu ya mabadilishano ya
kitamaduni ya wiki moja itakayohusisha kuwaleta nchini Tanzania Mwongozaji wa
Filamu wa Kimarekani Judd Ehrlich na mtaalamu wa filamu Debra Zimmerman kutoka
tarehe 9 hadi16 Julai, 2017. Hati hiyo
ya Makubaliano ilisainiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Virginia
Blaser na Mkurugenzi wa ZIFF Fabrizio
Colombo.
Judd Ehrlich ni muongozaji wa filamu
ya maisha na matukio halisia (documentary) iitwayo Keepers
of the Game, ambayo inaangazia jitihada za timu ya wasichana kutoka
makabila ya asili ya Marekani ikitafuta kushinda ubingwa wa mkoa wa mchezo
uitwao lacrosse, ambao kitamaduni
ulikuwa ni mchezo wa wanaume na wavulana tu.
Debra Zimmerman ni mtaalamu wa filamu na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi
iitwayo Women Make Movies (Wanawake
Watengeneza Filamu) ambayo imedhamiria kuongeza uwezo na fursa kwa wanawake
wanaohusika katika utengenezaji wa filamu.
Kupitia ubia na ZIFF, Ehrlich na Zimmerman watafanya kazi moja kwa moja na
watengeneza filamu wa Kizanzibari wanaochipukia wakati wa tamasha la 20 la
filamu la Zanzibar. Wataendesha warsha kadhaa kuhusu utengenezaji wa filamu za maisha na matukio halisia na
utafutaji masoko na usambazaji wa filamu pamoja na kuendesha warsha mahsusi
kuhusu ushiriki wa wanawake katika tasnia ya filamu.
Akizungumza katika hafla fupi ya
kusaini Hati ya Makubaliano, Kaimu Balozi Blaser alisema “tunafuraha kuimarisha
msaada wetu kwa watu wa Zanzibar kupitia programu hii ya mabadilishano ya
kitamaduni. Kwa pamoja tutatoa fursa kwa
watengeneza filamu wa Kimarekani na Kizanzibari kutumia sanaa hii kama nyezo ya
kushughulikia masuala mbalimbali yanayogusa jamii zao.”
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Virginia
Blaser na Mkurugenzi wa ZIFF Fabrizio wakitia sahihi hati hiyo ya Makubaliano (MOU) ya kuwa na programu ya mabadilishano ya kitamaduni ya wiki moja itakayohusisha kuwaleta nchini Tanzania Mwongozaji wa Filamu wa Kimarekani Judd Ehrlich na mtaalamu wa filamu Debra Zimmerman kutoka tarehe 9 hadi16 Julai, 2017.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Virginia Blaser na Mkurugenzi wa ZIFF Fabrizio wakibadilishana hati baada ya kutia hati hiyo ya Makubaliano (MOU)
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Virginia Blaser na Mkurugenzi wa ZIFF Fabrizio wakiongea na wanahabari baada ya kutia sahihi hati hiyo ya Makubaliano (MOU).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...