Wananchi wa kata ya Mpambala, wilaya ya Mkalama mkoani Singida wameiomba Serikali kuhakikisha inamaliza ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti haraka iwezekanavyo ili kurahisisha huduma za mawasiliano kati ya wilaya ya hiyo na mikoa jirani ya Simiyu, Manyara na Mara.

Wananchi hao wamemweleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, alipofika kukagua daraja hilo mkoani humo jana, ambapo pamoja na mambo mengine wamesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutatatua changamoto za usafiri hususan katika kipindi cha masika.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), mkoa wa Singida, Eng. Yohanes Mbegalo, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa kwanza kulia), kuhusu maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi wa Daraja la Sibiti lenye urefu wa M 82 linalounganisha Mikoa ya Singida, Simiyu, Manyara na Mara.

"Tunaomba Mheshimiwa Naibu Waziri utusaidie  kukamilisha daraja hili mapema ili  tupate huduma muhimu kama usafiri hasa kipindi cha masika", amesema mmoja wa wananchi.

Aidha, wananchi hao wameipongeza Serikali kwa kuendelea na jitahada za ujenzi wa barabara za maingilio zenye urefu wa KM 25 katika daraja hilo ambapo kwa sasa mradi wote umefika asilimia 43.9.

Kwa upande wake Naibu Waziri Eng. Ngonyani ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani humo kuhakikisha kuwa wanamsimamia mkandarasi na kuhakikisha anamaliza ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara hizo kufikia mwezi Machi mwakani.
Mhandisi Mshauri Mr. Sunil Singh, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (kulia), nguzo za Daraja la Sibiti zilizosimamishwa wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja hilo na barabara za maingilio kwa kiwango cha changarawe KM 25, mkoani Singida jana.

Kuhusu deni la mkandarasi huyo analoidai Serikali, Eng. Ngonyani amesema kuwa watahakikisha wanamlipa mapema ili kufanikisha mradi kumalizika kwa muda uliopangwa.

"Tutahakikisha tunalipa deni lote linalodaiwa ili kurahisisha mradi huu kuisha haraka kwa ajili ya wananchi kuweza kutumia daraja hili pamoja na barabara yake kwa kuwa ni kiungo muhimu kwao", amesisitiza Naibu Waziri.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...