Dar es Salaam, TANZANIA. Hapo tarehe 1 Mei 2017, mtuhumiwa wa usafirishaji wa dawa za
kulevya Ali Khatib Haji Hassan (“Shkuba”) na washirika wake wawili Iddy Salehe Mfullu na Tiko
Emanual Adam walisafirishwa kwenda nchini Marekani, kukabili mashtaka yao kuhusiana na
biashara haramu ya dawa za kulevya katika Mahakama kuu huko Huston, Texas. Watuhumiwa
hao watatu waliwasili nchini Marekani tarehe 2 Mei 2017. Kusafirishwa kwa watuhumiwa hao ni
matokeo ya ushirikiano mkubwa, wa karibu na wa muda mrefu baina ya serikali za Marekani na
Tanzania.
“Kupelekwa nchini Marekani kwa Hassan na washirika wake ni mafanikio yatokanayo na
ushirikiano wetu wa muda mrefu na wenzetu katika serikali ya Tanzania katika nyanja nyingi katika
sekta za usalama, usimamizi wa sheria na haki. Kesi hii ni mfano mzuri sana wa jinsi tunavyoweza
kuimarisha usalama wa kikanda na kimataifa pale tunapofanya kazi pamoja,” alisema Virginia
Blaser, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mamlaka za Tanzania zilimtia mbaroni Shkuba kwa tuhuma za usafirishaji dawa za kulevya
hapo mwaka 2014 baada ya msako wa miaka miwili uliofuatia kukamatwa kwa takriban kilo 210 za
dawa za kulevya aina ya heroine huko Lindi Tanzania mwezi Januari 2012. Tarehe 9 Machi 2016,
Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Wizara ya Fedha ya Marekani (U.S. Department of the
Treasury’s Office of Foreign Assets Control - OFAC) chini ya sheria ya kuwabainisha raia wa
kigeni walio vinara wa biashara ya dawa za kulevya (Foreign Narcotics Kingpin Designation
Act – Kingpin Act) ilimtaja Hassan na kundi lake kama raia wa kigeni aliye kinara wa biashara
hiyo haramu.
Kwa taarifa zaidi kuhusu tamko hilo la OFAC, tembelea
HAPA
Mwezi Machi 2016, Jopo la maafisa mashtaka (grand jury) la Huston, Texas, lilipitisha mashtaka
dhidi ya Shkuba na washirika wake kwa tuhuma za kula njama ya kumiliki kwa lengo la kusambaza dawa Za kulevya aina ya heroin nchini Marekani katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi
2015. Hatimaye serikali ya Marekani iliwasilisha ombi rasmi kwa Tanzania la kuwapeleka
watuhumiwa hao watatu nchini Marekani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...